Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Mchengerwa Atoa Maelekezo Mazito Baada ya Kupokea Taarifa ya HAKIMILIKI ya Wasanii na Mashujaa wa Madola
Aug 12, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na John Mapepele

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa ameliagiza Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kupitia upya kanuni kwa kuwashirikisha wadau wote wa Sanaa nchini Tanzania ili ziweze kuainisha bayana mfumo mzuri wa ufanyaji kazi unaowashirikisha wasanii binafsi, vyama, na mashirikisho ya Sanaa.

Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo usiku wa kuamkia leo Agosti 13, 2022 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam baada ya kupokea taarifa rasmi ya namna bora ya kusimamia HAKIMILIKI na Mirabaha kwa wasanii nchini kutoka kwa Kamati aliyoiteua Julai Mosi mwaka iliyoongozwa na Victor Tesha.

 “Mfumo huu utasaidia kuwatambua wasanii wote nchini na kuweza kuwahudumia kwa urahisi kwani mfumo uliopo sasa unatoa nafasi ya kila msanii kujitafutia riziki mwenyewe kitu kinachofanya wasanii wengi kukosa umoja na kuzalisha migogoro isiyokuwa na tija”. Amesisistiza Mhe. Mchengerwa.

Pia, ameliagiza BASATA kufanya mapitio na usuluhishi katika migogoro ya wasanii, ikiwa ni pamoja na kuandaa dawati la ushauri wa kisheria kuhusu Mikataba na masuala ya Sanaa.

Aidha, ameongeza kuwa masuala yanayohusu usimamizi wa hakimiliki ni mtambuka na yanahusisha Taasisi nyingi za Serikali na nyakati fulani zenye maslahi pingani, hivyo mapendekezo yaliyotolewa na Kamati ya kuwa na mfumo bora wa uendeshwaji wa Taasisi ya hakimiliki yatazingatiwa na Serikali ili kurekebisha mnyororo mzima wa kazi za sanaa nchini na hivyo kupelekea kutengeneza sekta ya sanaa iliyo na nguvu zaidi katika ukanda wa Afrika na dunia kwa ujumla.

Ameongeza kuwa Wizara ina mkakati wa uwezeshaji kwa kujenga majukwaa ya kuendeleza kazi za wasanii, kuwekeza katika “Digital Platform” ili wasanii wapate uwanja wa kuuza na kutangaza bidhaa zao. Pia kuratibu na kuweka kanuni mahususi kwa lengo la kuendeleza kuongeza thamani za kazi zote za Sanaa.

Wakati huo huo   Waziri Mchengerwa amekabidhi bonus ya Tshs 30,000,000 itakayogawanywa kwa wachezaji na benchi la ufundi lote lililoshiriki katika michezo ya Jumuiya ya Madola pamoja na  kuwapatia  fedha wachezaji watatu walioshinda medali kwenye mashindano  hayo.

Wachezaji hao ni Nahodha wa timu ya Tanzania, Bw. Felix Simbu aliyetwaa medali ya fedha na kunyakua dola 7500 na Mabondia Bw. Yusufu Changalawe na Bw.Kassim mbundwike waliotwaa medali za shaba ambao Serikali iliwapatia Dola za Kimarekani 5000 kila mmoja.

Katika kuhakikisha timu za Tanzania zinaendelea kufanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa, Mhe. Mchengerwa ameielekeza Idara ya Michezo na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuanza maandalizi haraka ya kuandaa Timu za Taifa kwa ajili ya maandalizi ya mashindano ya ALL AFICAN GAMES yatakayofanyika nchini Ghana katika mji wa Accra kuanzia tarehe 14 -18 Agosti 2023.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi