Na John Mapepele
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo na Mbunge wa Jimbo la Rufiji. Mhe, Mohamed Omary Mchengerwa ametoa vifaa vya michezo kwa shule zote za msingi na Sekondari na wanafunzi wanamichezo wote wanaoshiriki kwenye mashindano ya michezo kwa shule za Msingi (UMITASHUMTA) na Mashindano ya Shule za Sekondari (UMISSETA) kwa mwaka 2022 Wilaya ya Rufiji.
Mhe. Mchengerwa amekabidhi vifaa hivyo kwa Mkuu wa Wilaya ya Rufiji Julai 17, 2022 kwenye shule ya Sekondari ya Ikwiriri iliyopo Wilaya ya Rufiji ambapo amesema ameamua kufadhili vifaa hivyo katika Wilaya ya Rufiji ili kuiendeleza michezo kwa kuwa michezo ni biashara na ajira kubwa kwa vijana.
“Nimeamua kusaidia vifaa hivi kwa kuwa natambua kwa sasa michezo ni miongoni mwa chanzo cha ajira na biashara kubwa duniani hivyo ni vema kufanya michezo kwa umakini mkubwa ili kujipatia ajira” amefafanua.
Amewataka wachezaji hao kuwa na nidhamu na kujituma kwa kufanya mazoezi ili waweze kushinda kwenye mashindano mbalimbali.
“Nendeni mkajitume, michezo ni ajira na furaha wasikilizeni walimu wenu, hata shuleni mtafanya vizuri”amesisitiza Mhe. Mchengerwa.
Aidha amesema dhamira ya Serikali kwa sasa ni kuendeleza michezo ambapo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,. Mhe, Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa anazofanya kwenye michezo katika kipindi kifupi cha utawala wake ambazo zimeleta mapinduzi makubwa kwenye sekta hiyo.
Vifaa hivyo vimegharimu zaidi ya milioni 23 ambazo zimenunua zaidi ya jezi seti 200, trakisuti pea 100, kofia 200 na mipira 100.
Pia, amefadhili Ligi ya mpira wa miguu ya Sensa katika Wilaya ya Rufiji ambapo ametoa seti 6 za jezi kwa timu sita na mipira 12 kwa ajili ya mashindano hayo.
Amesema lengo la mashindano hayo ni kuhamasisha wananchi kushiriki kuhesabiwa kwenye sensa ya kitaifa yam waka huu kwa manufaa mapana ya wananchi wa Rufiji na Taifa kwa ujumla.
Aidha, amewahimiza wananchi wa Wilaya ya Rufiji na watanzania wote kujitokeza kwa wingi Agosti 23, mwaka huu kuhesabiwa kwenye zoezi la sensa kitaifa.
Mwenyekiti wa Halimashauri ya Wilaya ya Rufiji amemshukuru Mhe. Mchengerwa kwa jitihada zake na mchango wake kwenye sekta ya michezo ambapo amemhakikishia kuwa michango anayotoa itatumika vizuri ili kupata matokeo chanya.