Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Makamba Akutana na Ujumbe wa Benki ya Dunia, Wajadili Maendeleo Sekta ya Nishati
Mar 28, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Zuena Msuya DSM,

Waziri wa Nishati, January Makamba amekuta na ujumbe wa Benki ya Dunia ukiongozwa na Mkurugenzi Mkazi wa benki hiyo kwa upande wa Tanzania,  Mara Warwick  na kuzungumzia mambo mbalimbali kubwa likiwa ni uendelezaji wa Sekta ya Nishati ikiwemo masuala ya umeme na gesi.

Katika mazungumzo hayo, Makamba ameishukuru benki hiyo kwa ushirikiano wake kwa Serikali ya Tanzania pia kuwezesha utekelezaji wa miradi ya Maendeleo nchini ukiwemo ule wa kuinganisha Tanzania na Zambia (TAZA).

Mazungumzo hayo yamefanyika katika ofisi za Wizara hiyo zilizopo mkoani Dar Es Salaam, Machi 28, 2022, pamoja na mambo mengine mazungumzo hayo yamelenga zaidi kuimarisha ushirikiano kati ya benki hiyo na Serikali ya Tanzania  katika kuendeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Serikali ya Tanzania inaishukuru Benki ya Dunia kwa kuwezesha miradi ya nishati hapa nchini, tunawaahidi tutaendelea kushirikiana katika nyanja mbalimbali kwa kuwa tumeona matokeo chanya katika miradi ambapo benki hiyo imeiunga mkono hasa katika Sekta ya Nishati,” alisema Makamba.

Mkutano huo pia umehudhuriwa na Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Seif Said na Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Anitha Ishengoma pamoja na Viongozi wengine waandamizi kutoka Wizarani, REA na TANESCO.

Katika kikao hicho wamejadili mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini, njia kuu za kusafirisha umeme pamoja masuala ya gesi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Warwick amemueleza Waziri wa Nishati kuwa wataendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kwa kuiunga mkono sekta ya Nishati, ili kutanua wigo wa ukuaji wa maendeleo ya sekta hiyo.

Pia watawajengea uwezo wataalam wa kada hiyo ili kuweza kuongeza tija na ufanisi katika sekta hiyo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi