Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Mabula Awataka Wakurugenzi Halmashauri Kwenda na Kasi ya Rais Samia
Oct 02, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt Angeline Mabula amezitaka halmashauri nchini kwenda na kasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutenga ardhi kwa ajili ya uwekezaji.

Dkt. Mabula alitoa kauli hiyo oktoba 1, 2022 wakati akihitimisha kikao kazi baina ya Wakurugenzi wa Halmashauri na wataalamu wa sekta ya ardhi kikichofanyika jijini Dodoma.

Huku akimshukuru Mhe Rais Samia kwa kuipa kipaumbele sekta ya ardhi, Dkt. Mabula aliwaeleza washiriki wa kikao kazi kuwa, kinachohitajika kwa sasa ni kwenda na kasi ya Rais, Mhe. Samia hasa kwa kuzitaka halmashauri kujiandaa katika zoezi zima la uwekezaji.

"Hata kama mmetenga maeneo je mmeyatwaa na ni ya kwenu au mkipata muwekezaji ndiyo mnaanza kuhangaika, hapa  kinachohitajika ni kwenda na kasi ya Rais Samia, Wakurugenzi  ndiyo ninyi na Maafisa Ardhi ndiyo ninyi". Alisema Dkt. Mabula

Aliongeza kwa kusema kuwa, ardhi zilizotengwa kwa ajili ya uwekezaji katika halmashauri, Wakurugenzi wake wahakikishe wanazitwaa na kuwa mali ya Serikali ili iwe rahisi kumpatia Muwekezaji pale anapotokea.

Aidha, Waziri wa Ardhi alizungumzia suala la halmashauri kushikilia ardhi kwa muda mrefu bila kulipa fidia kwa wamiliki wake ambapo alisema pale halmashauri inaposhindwa kulipa fidia eneo ililolitwaa basi eneo hilo lirudishwe kwa mhusika na pale litakapohitajika ufanyike tena uthamini.

"Kuna ardhi mmezishikilia kwa miaka nenda rudi fidia hailipwi lakini mgogoro unakuja ardhi sasa tuseme ukishindwa kulipa fidia maana hiyo ardhi umrudishie mwenyewe ukitaka tena utafanya uthamini" alisema Dkt. Mabula.

Aliwaambia washiriki wa mkutano huo kuwa,  Serikali haitaki uonevu kwa wananchi kwa kuwa siyo maelekezo ya rais na kusisitiza kuwa Serikali inathamini wawekezaji hata wa ndani na pale wanapokuja wawekezaji wa nje wale wa ndani wasionekani siyo lolote.

Kikao kazi kati ya wakurugenzi wa halmashauri na wataalamu wa sekta ya ardhi mbali na mambo mengine kilijadili changamoto na kutoa maoni na ushauri kuhusu namna bora ya kusimamia watumishi wa sekta ya ardhi  nchini kwa lengo la kuwa na ufanisi na kwa maskahi mapana ya nchi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi