[caption id="attachment_35539" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani (katikati), akikata utepe kuashiria uwashaji rasmi wa umeme katika kijiji cha Dakama, wilayani Meatu, Mkoa wa Simiyu, Septemba 20, 2018. Kushoto kwake ni Mkuu wa Mkoa huo Anthony Mtaka na kulia kwake ni Mbunge wa Jimbo la Meatu, Salum Hamis Salum.[/caption]
Na Veronica Simba – SIMIYU
Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani ameeleza kukerwa na kasi ndogo ya Mkandarasi anayetekeleza Mradi wa Umeme Vijijini, Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Kwanza (REA III-Round 1), White City & Guangdong JV Ltd, katika Wilaya ya Meatu, mkoani Simiyu.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Dakama wilayani Meatu, wakati wa hafla ya uwashaji rasmi wa umeme katika eneo hilo, Septemba 20, 2018 Waziri Kalemani alisema kasi ya Mkandarasi huyo siyo ya kuridhisha.
“Nimekuwa ziarani katika mikoa mbalimbali na kote nilikopita nimekuta wakandarasi wakifanya kazi; hapa sijamkuta kazini, maana yake kuna shida.”
[caption id="attachment_35540" align="aligncenter" width="750"]Aidha, Waziri alisema alitarajia akute Yadi maalum ya Mkandarasi husika yenye kutumika kuhifadhia vifaa mbalimbali kama ilivyo sehemu nyingine, lakini haipo, jambo ambalo alisema linadhihirisha uwajibikaji duni wa Mkandarasi husika.
Akifafanua zaidi, alisema kuwa, hakuna anayepinga kuwa taratibu za utekelezaji wa Miradi husika hufanyika hatua kwa hatua, lakini siyo sababu ya kumfanya Mkandarasi kutokufanya kazi kwa kasi inayotakiwa.
Kufuatia hali hiyo; Waziri Kalemani alilazimika kumwagiza Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Raymond Seya kumwondoa katika nafasi hiyo, Meneja wa Shirika hilo Wilaya ya Meatu, Amos Mtae kwa kushindwa kumsimamia Mkandarasi, na kumteua Meneja mwingine mapema iwezekanavyo.
[caption id="attachment_35541" align="aligncenter" width="750"]Waziri alitoa agizo hilo baada ya Meneja husika kutoa maelezo yaliyoonesha hatekelezi vema majukumu yake, ikiwa ni pamoja na kutokuwa na tarifa ni wapi Mkandarasi anafanya kazi kwa siku hiyo na ni kwanini hana Yadi maalum ya kuhifadhi vifaa katika eneo hilo.
“Wakandarasi hawana vifaa, hawana Yadi ya kuhifadhia; wewe Meneja unakagua nini?! Wewe kama msimamizi wa Mkandarasi husika, hujui alipo leo, sasa unasimamia nini?!”
Waziri alisisitiza kuwa miradi ya umeme haina mzaha na kwamba Serikali kupitia Wizara yake, imedhamiria kuwapelekea wananchi wote umeme wa uhakika na kwamba itatekeleza jukumu hilo ndani ya muda uliopangwa. “Hatutakubali mtu yeyote aturudishe nyuma au kutuchelewesha.”
Mradi wa REA III Mzunguko wa Kwanza, ulianza kutekelezwa Juni 2017 na unatarajiwa kukamilika Juni 2019.
[caption id="attachment_35542" align="aligncenter" width="750"](Picha na Veronica Simba- Wizara ya Nishati)