Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo amehimiza wananchi jijini Mwanza kuzingatia matumizi sahihi ya vipimo kila mara wanapofanya manunuzi na kuuza bidhaa mbalimbali.
Aliyasema hayo Septemba 11, 2024 wakati akifungua rasmi Maonesho ya 19 ya Biashara ya Afrika Mashariki yanayofanyika katika Uwanja wa Furahisha jijini Mwanza.
"Wizi wa kuchezea vipimo ni kosa kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo Sura Na. 340 na hata vitabu vya dini vinakataza wizi wa vipimo," alisisitiza.
Katika hatua nyingine, akizungumzia ushiriki wa Wakala wa Vipimo (WMA) katika Maonesho hayo, Afisa Vipimo Mwandamizi Mkoa wa Mwanza, Lazaro Joram alisema ni mwendelezo wa utoaji elimu kwa umma kuhusu matumizi sahihi ya vipimo kwa wafanyabiashara waliopo ndani ya Mkoa wa Mwanza pamoja na nchi jirani.
"WMA tunatumia Maonesho haya ili kuwawezesha wadau wetu kutambua majukumu yetu, kueleza umuhimu wa kuhakiki na kutumia vipimo sahihi na kutoa ushauri wa kitaalamu juu ya matumizi ya vipimo pamoja na kuendelea kuwaelimisha kuhusu aina za vipimo vinavyopaswa kutumika katika biashara."
Joram aliwakaribisha wananchi kutembelea Banda la WMA ili kufahamu aina za mizani wanazoweza kutumia katika sekta za kilimo, uvuvi, biashara na usafirishaji.
“Tunazo aina nyingi za mizani lakini siyo kila mzani unaruhusiwa kutumika katika biashara au katika sekta ya kilimo hivyo ukitembelea Banda letu tutakupa elimu ya kutambua mizani sahihi iliyohakikiwa pamoja na kutambua alama zinazowekwa katika vipimo vilivyo hakikiwa,” alisema.
Akidadavua kuhusu elimu inayotolewa kwa wananchi wanaotembelea Banda la WMA, Joram alisema eneo mojawapo ni kuhusu namna sahihi ya ufungashaji wa mazao ya shamba ambapo kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo mazao yote yanatakiwa kufungashwa kwa uzito usiozidi kilogramu mia moja (100 kg) na endapo mkulima atafungasha mazao kwa uzito zaidi ya uliotajwa kisheria atakuwa amefungasha Lumbesa na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
“Kwa sasa tafsiri ya lumbesa ni uzito unaozidi kilo mia moja (100 kg) tofauti na awali ambapo ilikuwa inatafsiriwa kama kuongeza kifungashio juu ya gunia hivyo tunawahimiza wakulima kutumia mizani ili kujua uzito wa mazao wanayofungasha,” alisisitiza.
Akieleza zaidi, alisema kuwa, Kanda ya Ziwa kuna mazao ya kimkakati aina mbili ambayo ni Pamba na Kahawa ambapo jukumu la WMA ni kuhakiki mizani zote zinazotarajiwa kutumika kwenye ununuzi wa mazao hayo kabla ya msimu kuanza na baada ya kufanya uhakiki mizani iliyo sahihi huruhusiwa kutumika katika ununuzi wa mazao hayo.
Vilevile, alisema wakati wa ununuzi, WMA hufanya kaguzi za kushtukiza katika Vyama vya Ushirika vya Msingi (AMCOS) ili kujiridhisha kama mizani zinatumika kwa usahihi kama zilivyo hakikiwa ili kuwalinda wakulima.
Pamoja na majukumu mengine, WMA pia ina jukumu la kusimamia usahihi wa vipimo kwenye sekta ya usafirishaji ambao ni pamoja na usafiri wa anga, barabara na usafiri wa majini kwa kuhakikisha mizani zinazotumika ziko sahihi na zimehakikiwa ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza ikiwemo kubeba mizigo yenye uzito mkubwa ambayo inaweza kusababisha vyombo hivyo kuanguka na miundombinu kuharibika.
Kwa upande wake, Afisa Uhusiano Mwandamizi wa WMA anayeshiriki Maonesho hayo, Paulus Oluochi alitoa wito kwa wananchi kutembelea Banda la WMA ili kujifunza kuhusu matumizi sahihi ya vipimo lakini pia kuwasilisha changamoto mbalimbali kama zipo ili ziweze kupatiwa ufumbuzi.
Alisema endapo mwananchi yupo mbali, anaweza kuwasiliana na WMA kupitia nambari isiyo na malipo 0800 110097.
Maonesho hayo ya 19 ya Biashara ya Afrika Mashariki yanatarajiwa kufikia tamati Septemba 15, 2024.