Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Jafo Aridhishwa na Maendeleo Ujenzi wa Jengo la Ofisi ya Makamu wa Rais
Jun 22, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo amefanya ziara ya kukagua ujenzi wa jengo la Ofisi ya Makamu wa Rais katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma leo Juni 22, 2022.

Akizungumza mara baada ya kukagua jengo hilo, Dkt. Jafo alionesha kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa jengo huku akimtaka Mkandarasi Kampuni ya SUMA JKT kuongeza kasi ya ujenzi ili likamilike na hatimaye lianze kutumika.

Dkt. Jafo aliishukuru Kampuni ya SUMA JKT ambayo imepewa kazi ya kutekeleza mradi huo kwa hatua iliyopiga pamoja na kamati iliyoteuliwa kuusimamia ujenzi huo.

“Pamoja na kuwa mradi huu tunatakiwa tuukamilishe Novemba tisa mwakani lakini ikiwezekana hata ukamilike haraka zaidi naijapokuwa mkataba unasema kazi inaisha mwaka mmoja lakini ikiwezekana mwanzoni mwa mwakani iwe imekamilka,” alisema Jafo.

Hata hivyo Waziri huyo alitoa maelekezo kwa Wakandarasi wote wanaojenga majengo ya Serikali katika maeneo mbalimbali kuweka mfumo kuvunia maji ya mvua ili kunusuru athari za mafuriko pamoja na kuwa na hifadhi ya maji.

Awali akiwasilisha taarifa ya mradi huo, Karani wa Mradi wa Ujenzi,Bi. Philomena Bango alisema kazi mbalimbali zinaendelea kutekelezwa kulingana na mpango kazi (master program) uliowekwa.

Bi. Philomena aliongeza kwa kusema kuwa hadi kufikia sasa Mkandarasi ameshakamilisha kazi ya ujenzi wa mradi kwa asilimia 33 na kuwa wana matumaini utakamilika kwa wakati.

Hata hivyo, alisema kuwa Mkandarasi huyo anakabiliwa na changamoto ya kupanda kwa gharama za vifaa vya ujenzi vikiwemo ndondo.

Ofisi ya Makamu wa Rais ilisaini mkataba wa Shilingi bilioni 18.8 na Kampuni ya SUMA JKT wa kuanza ujenzi huo Oktoba 13, 2021 na kukabidhi rasmi eneo la ujenzi kwa Mkandarasi baada ya kushinda zabuni ambapo ujenzi wake unasimamiwa na Msimamizi Elekezi Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi