Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo ameendelea kuhimiza matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira kutokana na ukataji wa miti.
Ametoa rai hiyo alipokuwa akizungumza na Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC) wakati wa uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024 katika Uwanja wa Chuo cha Ushirika Moshi mkoani Kilimanjaro uliofanywa na Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa leo Aprili 02, 2024.
Dkt. Jafo amesema kuwa Serikali ilitangaza kusitisha matumizi ya kuni na mkaa kwa taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100 kuanzia Januari 2024 ambapo tayari taasisi hizo zimetekeleza maelekezo hayo.
Amesema kuwa kila mwaka takriban hekta laki nne za misitu zinapotea kutokana na kukatwa kwa ajili ya kuni na mkaa, hivyo Serikali inahamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kuinusuru.
“Utunzaji wa mazingira unagusa mambo mengi, hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan alizindua Kampeni ya Nishati Safi ya Kupikia ili kuhifadhi mazingira,“ amesisitiza.
Aidha, Waziri Jafo amesema kuwa Mwenge wa Uhuru mwaka huu umeleta faraja kubwa katika utunzaji wa mazingira kwani utakimbizwa mikoa yote hivyo utasaidia wananchi kuelewa dhana nzima ya utunzaji wa mazingira.
Itakumbukwa kuwa katika kilele cha Mwenge wa Uhuru 2023 kilichofanyika Oktoba 14 mkoani Manyara, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango alitoa rai kwa Ofisi ya Waziri Mkuu kuendelea kutumia ujumbe unaohamasisha jamii utunzaji wa mazingira ili kusaidia kulinda na kutunza Mazingira.
Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2024 una kaulimbiu "Tunza Mazingira na Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa Endelezu" ambayo inaweka msisitizo kwa namna nyingine katika uhifadhi wa mazingira.