Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Jafo Aanika Mafanikio ya Mwaka Mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita
Mar 02, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo ameelezea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kipindi cha mwaka mmoja leo Machi 2, 2022 jijini Dodoma.

Akizungumza na Waandishi wa Habari alisema kuwa katika kipindi cha mwaka mmoja wa Serikali, Ofisi ya Makamu wa Rais imeboresha mfumo na taratibu za utoaji wa vibali vya Tathmini ya Athari kwa Mazingira kwa kutoa miongozo ya namna ya kutekeleza agizo la utoaji wa vibali husika ndani ya siku 14 baada ya kupokea taarifa ya mwisho kutoka kwa Mwekezaji. 

Dkt. Jafo alisema kuwa katika kipindi hicho, jumla ya vibali 1445 vimetolewa ikiwemo vibali 1014 vya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) na vibali 431 vya Ukaguzi wa Mazingira.

Aliongeza kuwa katika Miradi ya Hifadhi ya Mazingira, Ofisi imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya hifadhi ya mazingira ikiwemo, Mradi wa Kurejesha Ardhi Iliyoharibika na Kuongeza Usalama wa Chakula Katika Maeneo kame ya Tanzania .

Mradi huu unatekelezwa katika Halmashauri za Micheweni (Kaskazini Pemba), Magu (Mwanza), Nzega (Tabora), Mkalama (Singida), na Kondoa (Dodoma). Katika kipindi husika, Mradi umetoa hatimiliki ardhi za kimila kwa wananchi 1,448,” alisema.

Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi Kupitia Mifumo Ikolojia, unaotekelezwa katika Halmashauri za Kaskazini A (Unguja), Mpwapwa (Dodoma), Simanjiro (Manyara), Mvomero (Morogoro) na Kishapu (Shinyanga). 

Pia, Mradi wa majaribio wa Kikanda wa Kukabiliana na Mabailiko ya Tabianchi katika Bonde la Ziwa Victoria (Adapting to Climate Change in Lake Victoria Basin) ambao unatekelezwa na nchi tano (5) ambazo ni Tanzania, Uganda, Burundi, Rwanda na Kenya. Kwa upande wa Tanzania, Mradi unatekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Mwanza kwa gharama ya Dola za Kimarekani 500,000 sawa na Shilingi bilioni 1.

Kwa upande wa Muungano alisema kuwa, vimefanyika vikao vya kujadili masuala ya Muungano katika ngazi mbalimbali ambapo hoja 11 kati ya 18 zimepatiwa ufumbuzi na kuondolewa kwenye orodha ya hoja za Muungano.

Dkt. Jafo alisema hoja zilizopatiwa ufumbuzi na kuondolewa kwenye orodha ya hoja na Muungano ni pamoja na uingizaji wa maziwa kutoka Zanzibar, Usimamizi wa ukokotoaji na ukusanyaji wa Kodi kwenye Huduma za Simu unaofanywa na Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRB).

Alitaja hoja nyingine kuwa ni Mkataba wa mkopo wa fedha za ujenzi wa Barabara ya Chake chake hadi Wete – Pemba, Mkataba wa mkopo wa fedha za Mradi wa Ukarabati wa Hospitali ya Mnazi Mmoja, Mkataba wa mkopo wa fedha za ujenzi wa Bandari ya Mpigaduri, Uvuvi kwenye Ukanda wa Uchumi wa Bahari Kuu.

Kwa mujibu wa Waziri Jafo ajira kwa watumishi wa Zanzibar katika Taasisi za Muungano; Mgawanyo wa mapato yatokanayo na Misaada kutoka Nje ya Nchi, Mapato yanayokusanywa na Uhamiaji kwa upande wa Zanzibar; Uteuzi wa Makamu Mwenyekiti wa Tanzania Revenue Appeal Tribunal (TRAT) kutoka Zanzibar; na Uteuzi wa Mjumbe wa Bodi ya Bima ya Amana (Deposit Insurance Board - DIB kutoka Zanzibar.

“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimeendelea kushirikiana katika miradi mbalimbali ya maendeleo na miradi na programu mbalimbali zinazendelea kutekezwa,” alisema.

Waziri huyo alibainisha kuwa miongoni mwa miradi na program ni pamoja na: Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili uliozinduliwa mwezi Februari, 2020 ambapo jumla ya shilingi bilioni 112.9 zitatumika Zanzibar.

“Katika kuimarisha ushirikiano ndani ya miezi 12 ya Serikali ya Awamu ya Sita vimefanyika vikao 21 na Sekta zilizokutana ni Sekta ya Nishati, Sekta ya Maji, Sekta ya Madini, Sekta ya Uchukuzi, Sekta ya Utumishi na Utawala Bora, Uratibu wa shughuli za Serikali, Sekta ya Viwanda na Biashara, Sekta ya Maliasili na Utalii, Sekta ya Afya, Sekta ya Kilimo, Sekta ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Sekta ya Ardhi, Sekta ya Fedha na Mipango na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi