Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Hasunga Abainisha Taarifa ya Uzalishaji Korosho, Serikali Yaingiza Zaidi ya Trilioni 3.3   
Apr 21, 2020
Na Msemaji Mkuu

 

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo

Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga ametoa taarifa ya uzalishaji wa zao la korosho katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli ambapo amebainisha kuwa uzalishaji wa korosho umefikia Tani 1,036,698.

Waziri Hasunga amesema kuwa kiasi hicho kimeipelekea serikali kuingiza zaidi ya Trilioni 3.3 na fedha za kigeni zaidi ya Dola Milioni 1139 za Marekani kwa kipindi cha miaka mitatu (2017-2019) hivyo zao hilo kuongoza kwa uzalishaji kuliko mazao yote nchini.

Katika kutekeleza Sera ya Viwanda ya Serikali ya Awamu ya Tano, Waziri Hasunga amesema kuwa viwanda vya kubangua korosho vimeongezeka kufikia 30 kutoka viwanda 21.

Kadhalika katika taarifa hiyo ameeleza kuwa uzalishaji wa korosho nchini umeongezeka kwani mpaka sasa jumla ya mikoa 20 inazalisha korosho ukilinganisha na mikoa mitano pekee kabla ya Serikali ya Awamu ya Tano kuingia madarakani.

Watanzania wengi wamehamasika na kilimo hicho ambapo mikoa hiyo imeamua kujishughulisha na zao hilo kutokana na umuhimu wake katika mapato ya wakulima na watanzania kwa ujumla wake.

Kwa mujibu wa Waziri Hasunga amesema kuwa takribani watanzania wanaokadiriwa kuwa 1,200,000 mpaka 1,600,000 wameajiriwa katika zao hilo jambo ambalo limewanufaisha na kuweza kujipatia kipato chao.

Hata hivyo amesema kuwa mafanikio hayo yametokana na namna ambavyo Serikali imetoa elimu kwa kina kuhusu namna bora ya kutumia viuatilifu, kuongeza uzalishaji na tija, kadhalika uwekezaji katika eneo la utafiti kupitia kituo cha Taasisi ya Utafiti wa kilimo cha Korosho cha Naliendele kilichopo mkoani Mtwara.

Amesema kuwa kituo hicho kimefanya kazi kubwa na nzuri ya kuhakikisha kuwa wakulima wanapata miche bora ya mikorosho, yenye uwezo wa kuongeza uzalishaji, zenye uwezo wa kustahimili ukame, na zenye uwezo wa kukinzana na magonjwa mbalimbali hivyo kuwa kitovu cha uzalishaji wa miche ya mikorosho nchini.

Waziri Hasunga amesema kuwa katika kipindi hicho ubora wa korosho umeimarika hivyo kupelekea korosho ya Tanzania kupendwa na kuvutia wanunuzi wengi Duniani.

Kuhusu sekta ya ushirika, Waziri Hasunga amesema kuwa sekta hiyo imekuwa muhimu kwa watanzania kwani manufaa ya zao la korosho yanatokana na uwepo wa ushirika hivyo ushirika huo utaendelea kuimarishwa ili kuwa na mafanikio makubwa zaidi katika sekta hiyo.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi