Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Dkt. Mabula Ataka Clinic za Ardhi Kutatua Changamoto za Ardhi
May 29, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Munir Shemweta, WANMM DODDOMA

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt Angeline, Mabula amewataka Makamishna wa Ardhi Wasaidizi wa Mikoa nchini kuanzisha Clinic za Ardhi kwa ajili ya kushughulikia changamoto za sekta ya ardhi katika mikoa yao.

‘’Mjiwekee utaratibu mzuri wa kusikiliza changamoto za ardhi katika mikoa yenu kwa kuanzisha Clinic za ardhi, Mwanza wamekuwa wakifanya hivyo na wamefanikiwa’’ alisema Dkt Mabula

Kwa mujibu wa Dkt. Mabula, mbali na Wizara yake kufanya vizuri kwa baadhi ya mambo lakini kuna changamoto ya kutokuwa makini kwa watendaji na kutolea mfano wa barua za malalamiko zinazokwenda kwenye ofisi yake kuwa zingeweza kushughulikiwa katika mikoa husika.

‘’Changamoto kubwa hatuko makini, barua za malalamiko ya migogoro ya ardhi zinakuja kwa waziri na mimi nazirudisha kwenu kupata ufumbuzi na huko napata majibu, kwanini msingeshughulikia mpaka zije huku? ndiyo maana migogoro inakuwa mingi’’ alihoji Waziri Dkt Mabula.

Waziri wa Ardhi alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara, Makamishna wa Ardhi Wasaidizi wa Mikoa na watendaji wa Makao Makao Makuu mara baada ya kupitishwa kwa Bajeti ya Wizara yake na Bunge ambapo kiasi cha shilingi 110,323,474,000 kiliidhinishwa kwa mwaka wa fedha 2022/2023. 

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, sehemu kubwa ya migogoro ya ardhi inachangiwa na kutokuwepo mipango ya matumizi bora ya ardhi kwenye halmashauri hivyo aliwataka Makamishna wa Ardhi Wasaidizi wa Mikoa kuzikumbusha halmashauri katika mikoa yao kutenga fedha kwa ajili ya mipango hiyo.

Aidha, aliwataka pia kuhakikisha fedha ambazo halmashauri zinazokopeshwa kwa ajili ya miradi ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na ile faida inayopataikana itumike kuboresha sekta ya ardhi.

Kuhusu urasimishaji makazi holela, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliwataka Makamishna wa Ardhi Wasaidizi wa Mikoa kuhakikisha makampuni yaliyoshindwa kukamilisha kazi za urasimishaji yanachukuliwa hatua na kuangalia namna bora ya kukwamua kazi zilizokwama.

‘’Kama wao wamekwama kukamilisha kazi za urasimishaji ninyi mnafanyaje? Undeni timu katika mikoa kwenda wilaya moja hadi nyingine kulingana na mahitaji, zoezi hili lina chanagamoto kubwa sana mfano mkoa wa Tabora umefanya vizuri sana’’ alisema Dkt. Mabula.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwani Kikwete alikemea ucheleweshaji hati kwa wamiliki wa ardhi na kueleza kuwa, kama kuna tatizo linalosababisha mwananchi kutopata hati yake haraka basi aelezwe badala ya kumuacha mpaka aanze kulalamika.

‘’Kuna kilio cha wananchi cha hati kuchukua muda mrefu, nina mfano wa Dar es Salaam kuna mama mmoja hati yake ilichukua miaka saba na tatizo lake ilikuwa kitambulisho cha NIDA lakini hakuelezwa hadi akaja kulalamika kwangu, kama lipo tatizo mhusika aelezwe mapema, maduhuli yanakosekana kutokana na wananchi kutopewa hati’’, alisema Ridhiwani.

Dkt Allan Kijazi, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi alieleza kuwa, ipo changamoto kwa baadhi ya watumishi kufanya kazi bila kufuata taratibu na taarifa zao hazitolewi na Makamishna wa Ardhi wa Mikoa husika jambo alilolieleza kuwa, linalosababisha wizara kupata taarifa kupitia vyanzo vingine,

‘’Kuna changamoto ya watendaji kufanya kazi bila kufuata taratibu na taarifa hazipatikani na pale zinapopatikana ni kutoka katika vyanzo vingine sasa utendaji wenu utapimwa pia na jinsi unavyosimamia watendaji wako’’ alisema Dkt. Allan Kijazi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi