Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Bashungwa Atoa Siku Tano Wakuu wa Mikoa Kuwasilisha Taarifa za Ujenzi wa Madarasa 15,000
Jan 20, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Mwandishi Wetu

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Innocent Bashungwa amewaelekeza Wakuu wa Mikoa nchini kuwasilisha taarifa za ujenzi wa vyumba vya madarasa 15,000 kabla au ifikapo Januari 25, 2021.

Waziri Bashungwa ameyasema hayo leo Januari 20, 2022 jijini Dodoma wakati akifungua kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) linalofanyika kwa siku mbili mkoani humo likiwa na jumla ya Wajumbe 68.

“Natoa wito kwa Wakuu wa Mikoa kujiridhisha na taarifa hizo kwa kupitia taratibu na miongozo iliyotolewa na kuangalia kama thamani ya fedha katika ujenzi wa vyumba vya madarasa hayo imepatika”, alisema Waziri Bashungwa.

Amesema kwamba, Rais Samia Suluhu Hassan ameonesha ari ya kuboresha elimu ya awali, msingi na sekondari nchini kwani katika kipindi cha muda mfupi amewezesha ujenzi wa madarasa 15,000 yakiwemo madarasa 12,000 ya shule za sekondari na madarasa 3,000 kwa ajili ya vituo Shikizi vya shule za msingi hali itakayosaidia kuondoa changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa kwa wanafunzi.

Akizungumzia kuhusu Baraza hilo, Waziri Bashungwa amesema kuwa, katika mambo ambayo yatafanyiwa maboresho katika Tume hiyo ni kuimarisha na kuipa nguvu Tume ili iweze kuwahudumia Walimu nchini na kuboresha taaluma ya Ualimu ikiwa ni maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan.

Waziri Bashungwa ametumia nafasi hiyo kuipongeza Tume kwa kuwa na Baraza la Wafanyakazi lililo hai ambapo anaamini kuwa kwa siku mbili walizokutana hapo wamejadili masuala yote yaliyopangwa, wamejenga uelewa na kutafuta ufumbuzi.

Pamoja na hayo, ameitaka Tume ikaboreshe usimamizi wa Watumishi wa Walimu katika masuala ya ajira, nidhamu na maendeleo yao, pia ameziagiza Halmashauri zote nchini kubandika kwenye mbao za matangazo namba maalum ya kutuma malalamiko hayo ili waweze kuboresha huduma kwa wananchi wakiwemo Walimu.

Kwa upande wake Katibu wa Tume hiyo, Paulina Nkwama, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake katika kuinua sekta ya elimu pia, ameipongeza Wizara ya TAMISEMI kwa ubunifu mkubwa walioufanya kwa kutengeza Muongozo wa Kalenda ya Utekelezaji wa Mtaala.

Aidha, amezitaja baadhi ya changamoto za Tume hiyo zikiwemo za kukosekana kwa Makatibu Wasaidizi wa Wilaya, Bajeti isiyotosheleza, upungufu wa vitendea kazi pamoja na Watumishi huku akisistiza kuwa Tume hiyo itaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali ikiwemo suala la kukabiliana na janga la UVIKO 19 pamoja na kushiriki katika Sensa ya Watu na Makazi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi