Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wazazi, Walezi Kuwajibishwa Kisheria Suala la Watoto wa Mitaani
Sep 06, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Wazazi na walezi wametakiwa kuhakikisha wanawajibika katika suala la Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto kwa kuhakikisha kuwa Mtoto anatunzwa na kulindwa ili kumuepusha na mazingira hatarishi yatakayopelekea kufanyiwa vitendo vya ukatili vinginevyo watawajibishwa kisheria.


Hayo yamesemwa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima wakati akifungua Mkutano wa wadau wa Huduma za Ustawi wa Jamii nchini unaofanyika kwa siku mbili kuanzia tarehe 06-07, Septemba, 2022 mkoani Dar es salaam.


Waziri Gwajima amesema kuanzia sasa kila mtoto anayeishi na kufanya kazi mitaani atakayerudishwa nyumbani,  mzazi au mlezi ahakikishe ametoa taarifa kupotea kwa mtoto wake akiwa na namba ya Taarifa ya Polisi  (RB Number) aliyotoa taarifa siku aliyopotelewa na mtoto wake kinyume na hapo hatua za kisheria zitachukuliwa kwa uzembe na kutowajibika katika malezi.  

"Kifungu cha 8 na 9 cha Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009, kinampa majukumu mzazi na mlezi kuwajibika katika matunzo, malezi na ulinzi kwa mtoto hivyo  kifungo hicho kinatoa adhabu ya shilingi milioni tano (5)  au kifungo cha miezi isiyozidi sita au vyote kwa pamoja kwa mzazi/mlezi atakayekiuka sheria hii" amesema Mhe. Dkt. Gwajima.


Aidha, Waziri Dkt. Gwajima ameliomba Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Mahakama, kuchukua hatua kali dhidi ya Wazazi na Walezi wote watakaothibitika kisheria kukiuka kanuni hizo za maadili ya malezi ya watoto na usafirishaji wa watoto. 


"Ieleweke kwamba watoto wa leo ndio wazazi wa kesho, hivyo tusipowajibika sasa, tutakuwa na Taifa la wananchi wasiowajibika hapo baadaye", amesisitiza Waziri Dkt. Gwajima. 


Amewaelekeza pia Maafisa Ustawi wa Jamii wa Mikoa na Halmashauri kusimamia kikamilifu ufuatiliaji kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na Maafisa kazi kama ilivyoelezwa katika Kifungu cha  20 na kifungu cha 86 cha Sheria ya Mtoto ili kuondokana na tatizo la Watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Mhe. Amos Makala amesema Maafisa Ustawi wa Jamii hivi sasa wanatakiwa kufanya kazi za msingi za taaluma yao kwa sababu taaluma hiyo ndiyo msingi wa Taifa katika kumjengea na kumlinda mtoto katika ukuaji wake ili kuwa na jamii yenye kujitambua na kuwajibika kwa vizazi vijavyo. 


Mhe. Makala amesema yupo tayari kushirikiana na Wizara katika kutatua changamoto ya Makundi Maalum hasa watoto wanaoishi mazingira hatarishi kwa kuweka mipango na mikakati itayosaidia kupunguza kama sio kumaliza kabisa tatizo hilo.


"Tumejipanga na tuliahidi tutatafuta eneo Kigamboni kwa ajili ya kuwekeza katika miradi ya kuwawezesha kiuchumi Makundi Maalum" amesema Mhe. Makala.


Naye Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Zainab Chaula amesema watoto wana wazazi wao lakini inasikitisha kuona wanakumbana na mazingira magumu mitaani kwani mitaa haina Watoto, hivyo Jamii inatakiwa kuwajibika katika kuwalea na kuwalinda Watoto wasipatwe na vitendo vya ukatili katika ukuaji wao.


Dkt. Chaula amesema kazi ya Serikali ni kutengeneza Sera, Kanuni na Miongozo, hivyo ni wajibu wa wadau wote kushirikiana kutekeleza ili kuweza kufanikisha suala la Malezi Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto limazingatiwa na kupewa kipaumbele katika jamii. 
"Wizara inafanya kazi kubwa kuhakikisha wananchi wote wanakuwa na ustawi tunawekeza katika uchumi wa watu hawa namna gani tutakusanya rasilimali fedha kuyasaidia Makundi yote yaweze kujitegemea kiuchumi" amesema Dkt. Chaula.


Meneja mradi wa ACHIEVE Levina amesema kama wadau wanazingatia miongozo inayowekwa na Serikali katika utekelezaji wa Masuala ya Ustawi wa Jamii na wataendelea kuhakikisha matokeo yanaonekana.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi