Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Watumishi Waaswa Upendo, Uadilifu, Kufanya Kazi kwa Bidii na Ushirikiano - Mpwapwa
Oct 26, 2023
Watumishi Waaswa Upendo, Uadilifu, Kufanya Kazi kwa Bidii na Ushirikiano - Mpwapwa
Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma (aliyesimama), Bw.Ally Gugu akizungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa kabla ya kupokea taarifa ya Ukaguzi na Ufuatilia wa miradi ya maendeleo kwa kipindi cha Julai hadi Septemba 2023 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa tarehe 25 Oktoba, 2023.
Na Administrator

Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Mkoa wa Dodoma, wameaswa kufanya kazi kwa umoja na ushirikiano ili kuwezesha miradi ya kimaendeleo inayotekelezwa na Halmashauri hiyo kuwa na tija na ufanisi mkubwa.


Rai hiyo imetolewa tarehe 25 Oktoba, 2023 na Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma, Bw.Ally Gugu wakati wa ziara yake ya kikazi katika Halmashauri hiyo yenye lengo la kutathmini utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

"Mfanye kazi kama timu moja kwa kushirikianisha mambo na muwe na muunganiko na huo ndio upendo , taarifa za miradi zinapokuja mshirikishane isiwe ya mtu mmoja", ameeleza Gugu.

Aidha, Amesisitiza suala la usimamizi wa mapato ya Halmashauri na kusema ni lazima kusimamia kwa uaminifu fedha zikusanywe na kupelekwa sehemu husika pamoja na kutafuta mbinu nyingine za vyanzo vya mapato na zaidi ya yote ni kusimamia kwa uaminifu matumizi ya fedha za Serikali.



"Lazima muwe na mkakati madhubuti ya kusimamia mapato yaliyopo lakini kuzalisha vyanzo vipya vya mapato na kuvisimamia, fedha zikusanywe na zipelekwe kwa wakati sehemu husika kwa kuzingatia sheria na taratibu za matumizi husika," ameongeza.

Katibu Tawala Mkoa pia amegusia suala la afya na kuwataka watumishi kuchukua tahadhari kwenye afua za maradhi ili kujiepusha na yale yanayoepukika pamoja na kuzingatia lishe bora.

Kwa upande wake, Mkurungezi Mtendaji wa Halmashauri ya Mpwapwa, Bi. Mwanahamisi Ally amemuahidi Katibu Tawala Mkoa kutekeleza maelekezo yote aliyotoa na kumuhakikishia kutoa taarifa kwa wakati.



Awali Bw. Gugu alianza na kikao cha pamoja cha tathmini ya miradi na vyanzo vya mapato ya ndani ya Halmashauri na Wakuu wa Idara kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na baada ya hapo alifika katika Shule mpya ya Sekondari ya Kimagai, Hospitali ya Wilaya ya Mpwapwa na Shule ya Sekondari ya Mazae kwa ajili ya ukaguzi na utekelezaji wa maendeleo ya miradi.

Pia, miradi hiyo mitatu kwa maana ya ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Kimagai, ujenzi wa Jengo la Huduma ya Mama na Mtoto katika Hospitali ya Wilaya, vyumba 9 vya madarasa, mabweni 4 na matundu kumi na nne ya vyoo unaogharimu zaidi ya shilingi bilioni moja.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi