Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Watumishi Mpigachapa  Mkuu wa Serikali  Waaswa Kuzingatia  Ufanisi  
Jul 04, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na.Mwandishi Wetu

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uratibu) Prof.Faustin Kamuzora amewataka watumishi wa Idara ya Mpigachapa Mkuu wa Serikali kuzingatia ubora na ufanisi katika uchapaji wa nyaraka za Serikali.

Prof. Kamuzora ametoa wito huo leo jijini Dodoma alipotembelea Idara hiyo ili kuangalia namna wanavyoendesha shughuli zao.

Prof. Kamuzora alieleza umuhimu wa kuendelea kuwa na ubunifu katika utendaji kwa kuzingatia unyeti wa nyaraka za Serikali wanazochapisha na kuongeza wigo wa uzalishaji kwa kuwa na machapisho yenye ubora na viwango vya kuendana na soko ili kuongeza mapato ya nchi.

“Niwaombe watumishi wote mzingatie uzalishaji wenye tija kwa kuchapisha nyaraka zenye ubora na ufanisi utakao saidia kuongeza mapato ya nchi hivyo ni vyema kuwa na ubunifu wa hali ya juu,”alisema Prof. Kamuzora

Pamoja na maagizo hayo aliwasisitiza kuzingatia uzalendo wa nchi yao kwa kuwa waadilifu katika kuitumikia kwa uaminifu bila kutoa siri za Serikali.

“Ni lazima mzingatie maadili ya utumishi wa umma kwani idara hii ni nyeti inayoshughulika na uchapaji wa nyaraka za Serikali hivyo ni lazima kuwa na namna bora ya uendeshaji wa shughuli zenu kwa kuaminiana na kila mmoja kuwa mlinzi wa mwingine,”alisisitiza Prof. Kamuzora

Kwa upande wake Kaimu Mpigachapa Mkuu  wa Serikali Bw. John Kaswalala alimpongeza Katibu Mkuu kwa kuona umuhimu wa kuitembelea Idara hiyo, na kuahidi kuyafanyia kazi maagizo aliyotoa kwa lengo la kuboresha utendaji wa Idara ili kuwa na uzalishaji wenye tija na kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia.

“Kipekee nikushukuru kwa kuona umuhimu wa kuitembelea idara hii na kujua mazingira na changamoto za kiutendaji, nimefarijika kwa hatua hii hivyo tumeyazingatia maagizo yote tutayatekeleza ili kuendana na soko na mabadiliko ya kiteknolojia nchini,”alisisitiza Kaswalala.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi