Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Watumishi DUWASA Watakiwa Kuzingatia Maadili, Nidhamu ya Kazi
Jan 20, 2021
Na Msemaji Mkuu

Na Redempta Ndubuja - DODOMA

Naibu Waziri wa Maji Mhe. Maryprisca Mahundi amewataka watumishi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Dodoma (DUWASA) kuzingatia maadili na nidhamu katika utendaji kazi wao ili kuongeza ufanisi.

Mhe. Mahundi ameyasema hayo leo kwenye hafla ya uzinduzi wa Baraza la Sita la Wafanyakazi wa Mamlaka hiyo iliyofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Takwimu.

“Kuongezeka kwa ufanisi katika utendaji kazi kunatokana na kuzingatia maadili ya utumishi wa umma kama yalivyoainishwa kwenye miongoz mbalimbali, hivyo nawataka mhakikishe mnazingatia maadili” amesema Mhe. Mahundi.

Aidha, Mheshimiwa Naibu Waziri amewataka watumishi wa DUWASA kutumia  Baraza hilo kuweka mikakati imara ya kuhakikisha wanawatumikia wananchi.

“Ninaamini kwamba kupitia vikao mbalimbali wataweza kuimarisha utendaji kazi katika maeneo yao na kutetea maslahi ya watumishi” amesema Mhe. Mahundi.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi Aron Joseph amesema wafanyakazi wa mamlaka hiyo itayafanyia kazi maagizo ya Mheshimiwa Naibu Waziri ili kuweza kufikia malengo yao.

“Tutaendelea kuzingatia maelekezo hayo ili kufikia azma tuliyojiwekea…tunaamini tukiongeza kasi ya uwekezaji tutafikia azma yetu ya kuhakikisha kila mmoja anapata moja” amesema Mhandisi Joseph.

Kwa mujibu wa Ilani inayotekelezwa na Serikali iliyopo madarakani, Rais Dkt. John Pombe Magufuli ametekeleza jumla ya miradi ya maji 1,423 vijijini na mijini ikiwemo miradi 1,268 ya vijijini na miradi 155 ya mijini.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi