Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Watendaji Wazembe TANESCO Kuanza Kuchukuliwa Hatua Kila Mwezi - Dkt. Biteko
Apr 05, 2024
Watendaji Wazembe TANESCO Kuanza Kuchukuliwa Hatua Kila Mwezi - Dkt. Biteko
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akitazama namna Kituo cha Huduma kwa Wateja kinachosimamiwa na TANESCO kinavyopokea simu na kuhudumia wananchi wakati alipotembelea kituo hicho tarehe 4 Aprili, 2024 jijini Dar es Salaam.
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameagiza ripoti ya taarifa kila wiki ya Kituo cha Huduma kwa Wateja ya  Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ianze  kutolewa kila mwezi ili kufahamu maeneo yenye changamoto ya umeme nchini na kurahisisha watendaji wazembe kuchukuliwa hatua kwenye maeneo hayo.

 

Dkt. Biteko ametoa agizo hilo wakati wa ziara kwenye kituo hicho cha huduma kwa wateja leo tarehe 4 Aprili, 2024 jijini Dar es Salaam na kutoa maagizo mbalimbali yenye lengo la kuongeza ufanisi wa kituo hicho muhimu kwa wananchi nchini.

 

"Wateja wote wanaopiga simu kwa sababu mnaletewa matatizo ya wananchi ni lazima mtengeneze kila wiki tupate ripoti ni mkoa gani wanahudumiwa wateja kwa haraka na mkoa upi haupewi huduma kwa haraka ili tuchukue hatua," amesisitiza Dkt. Biteko.

Ameagiza kila mkoa uliopo chini ya TANESCO ufanyiwe tathmini kujua umeme umekatika mara ngapi na kufahamu sababu zilizopelekea umeme kukatika katika maeneo hayo ili kama ni uzembe umefanyika Serikali iweze kuchukua hatua haraka.

 

"Mimi ninafahamu kuna wakati umeme unakatika sio kwa sababu ya matatizo makubwa bali ni kwa matatizo madogo madogo ya kiusimamizi kwenye laini zetu. Unakuta kuna mahali mti umedondoka kwenye njia zetu na unachukua muda mrefu kuondolewa, au mteja amepiga simu anachukua muda kuhudumiwa, tunahitaji hiyo ripoti," amesisitiza Dkt. Biteko.

 

Katika hatua nyingine Dkt. Biteko ameagiza, kituo kuangalia utaratibu wa namna nzuri ya wateja kutogharamia malipo kipindi wanapopiga simu kuhudumiwa na kituo.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akimsikiliza Kaimu Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja TANESCO, Martin Mwambene akieleza namna Kituo cha Huduma kwa Wateja katika Shirika hilo kinavyopokea  simu  za wananchi na kuhudumia wakati alipotembelea kituo hicho leo tarehe 4 Aprili, 2024 jijini Dar es Salaam.

"Kiu yangu ni kuona kwamba tunakuwa na mfumo wa kupiga simu kwa wateja bila ya kuwaingiza kwenye gharama kwa sababu kuwaingiza kwenye gharama haina maana yoyote kwa wanachi," ameongeza Dkt. Biteko.

 

Dkt. Biteko amemuagiza Meneja wa Kituo hicho kuhakikisha taarifa ya Maendeleo ya kituo hicho kwa kila mkoa inawasilishwa kwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati ili kuongeza ufanisi wa watendaji nchini na asipofanya hivyo atafanyiwa mabadiliko katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia sasa.

Vile vile, ameagiza TANESCO kuhakikisha inajenga taswira nzuri ya nchi kupitia watendaji wa Shirika hilo kupitia kituo hicho. Amesema fedha zilizotolewa na Serikali za dharura kiasi cha shilingi bilioni 2.9 watu wahudumiwe ili kufurahia kuwa Watanzania kwa kupata huduma bora

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi