Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Watanzania Tujivunie Muungano Wetu; Msuya
Apr 06, 2024
Watanzania Tujivunie Muungano Wetu; Msuya
Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais Mstaafu, Mhe. Cleopa Msuya akizungumza Aprili 6, 2024 wakati alipotembelewa na Waandishi wa Habari nyumbani kwake jijini Dar es Salaam ambao walitaka kupata uzoefu wake wa uongozi na mtazamo wake hususan wakati huu ambao Tanzania inaenda kuadhimisha miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Na Mwandishi Wetu, Maelezo

Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais Mstaafu, Mhe. Cleopa Msuya amesema Tanzania inapoelekea miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni jambo la kujivunia kwa Watanzania wote.

Alisema kwamba kizazi cha Watanzania walioushuhudia muungano huo kinakwisha na kwamba kizazi kilichopo sasa kimezaliwa ndani ya muungano na sasa kazi iliyopo ni Watanzania wote kuendelea kuulinda na kuuimarisha muungano huo.

Mhe. Msuya aliongea hayo Aprili 6, 2024 wakati alipotembelewa na Waandishi wa Habari nyumbani kwake jijini Dar es Salaam ambao walitaka kupata uzoefu wake wa uongozi na mtazamo wake hususan wakati huu ambao Tanzania inaenda kuadhimisha miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Watanzania tujivune kwamba muungano wetu umedumu miaka 60, kazi yetu tuimarishe na tutumie muungano huo ili kuona vitu vinavyoweza kuleta faida kwa wananchi wa pande zote mbili kama ambavyo wenzetu kule walikuwa na changamoto ya umeme, hivyo ulipelekwa kutoka huku na sasa hawana tena changamoto hiyo,”alisema Mhe. Msuya.

Alisema, chombo chenye dhamana kijenge mifumo endelevu ya kuelimisha watu kuhusu muungano huo kikiwahusisha kundi la vijana kwa kushirikiana na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU), vilevile alishauri kwamba mfumo wa elimu uangaliwe ili elimu hiyo itolewe kwenye mambo ambayo yanajitokeza pande zote za muungano.

“Tuwe na mtazamo chanya na tuwe na chombo ambacho kitajenga hoja za masuala ya muungano wetu pamoja na faida zake, tujiulize tunawezaje kukitumia chombo hicho kikatuletea faida zaidi kwa Watanzania wa Bara na wa Zanzibar, ni lazima rasilimali zetu zitumike kuondoa shida na kuongeza matumaini kwa wote kwa mfumo unaokubalika”, alisema Mhe. Msuya.

Akitoa rai kwa Watazania wote, Mhe. Msuya alisema kwake yeye muungano ni jambo zuri na lenye faida nyingi ambazo zinaweza zisionekane kwa wote na kwamba si nchi zote zilizojaribu kuungana zilifanikiwa, wengi walishindwa hivyo kuwataka watanzania watembee kifua mbele.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi