Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wataalam wa Makumbusho Wapelekwe Dubai Wakajifunze Teknolojia – Mama Samia
Oct 04, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na:  Prisca  Libaga,MAELEZO, Arusha.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe ameagizwa kuwapeleka jijini Dubai maafisa wa Makumbusho mpya ya Olduvai Gorge kwa ajili ya mafunzo zaidi ya kiteknolojia.

Agizo hilo limetolewa na Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan wakati akizindua rasmi Majengo ya Makumbusho mapya ya Olduvai Gorge yaliyopo ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Mama Samia amesema Tanzania tumebarikiwa kwa kuwa na Makumbusho kubwa zaidi barani Afrika yenye kuweza kutoa historia ya Zamadamu, yaani binadamu wa kale, Maisha na zana zake; lakini hii itakuwa bora zaidi ikiwa tutaifanya iwe kiteknolojia zaidi.

“Tanzania tumebarikiwa na kuwa na makumbusho kubwa zaidi barani Afrika yenye kuweza kutoa historia ya binadamu wa kale (zamadamu),maisha na zana zake, nah ii tunayoizindua leo itakuwa bora zaidi ikiwa tutaifanya iwe kiteknolojia” alisisitiza Mama Samia.

Makamu wa Rais, ameongeza kuwa anayoimani kuwa Waziri Maghembe kupitia mahusiano mazuri aliyonayo na nchi za Saudi Arabia, atafanikisha suala la kuwapeleka wataalamu kwenda kupata mafunzo zaidi Dubai.

Aidha ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kujenga makumbusho kwenye maeneo mengine ya kihistoria kama Kilwa, Amboni (Tanga), Bagamoyo na Zanzibar kwa kuwa muelekeo wa sasa wa watu wengi duniani ni kurudi nyuma wajionee jinsi dunia ilivyokuwa zamani.

Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Maghembe alisema Makumbusho ya Olduvai Gorge ni ya pekee duniani ambapo karibu kila zana za kale, mabaki ya zamadamu na alama halisi zilizoachwa na binadamu zaidi ya miaka milioni 4 iliyopita, vinapatikana na kuongeza kuwa hakuna makumbusho kama hii ulimwenguni kote.

Naye Mbunge wa Ngorongoro, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Ole Nasha ameuomba uongozi wa Wilaya ya Ngorongoro pamoja na Mamlaka ya Hifadhi kuangalia suala la matumizi bora ya ardhi katika eneo hilo ambalo lina mchanganyiko wa hifadhi ya wanyamapori, wafugaji wa jamii ya Kimasai na eneo la historia ya mambo ya kale.

Kwa upande wake Meneja wa Urithi wa Utamaduni katika Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro, Mhandisi Joshua Mwankunda amesema Makumbusho ya Olduvai ni moja to kati ya mipango mingine mikubwa inayotarajiwa katika eneo hilo, ukiwemo ule wa Makumbusho mengine makubwa yatakayojengwa katika eneo jirani la Laetoli ambako nyayo za binadamu wa kale aliyeishi eneo hilo miaka milioni 4 iliyopita zinapatikana.

Mradi wa Makumbusho hayo umejengwa kwa gharama ya shilingi 1.7 Billioni/- huku asilimia 80 ya gharama hizo zikiwa ni ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU) na kiasi kilichobaki kikiwa ni fedha kutoka serikali ya Tanzania.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi