Takriban washiriki 200 wa Kongamano la 10 la Jotoardhi Afrika (ARGeo-C10) wamepewa mafunzo ya awali ya siku mbili ikiwa ni sehemu ya programu ya Kongamano hilo linalofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Oktoba 21 - 27, 2024.
Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga amefungua mafunzo hayo ya awali yanayohusiana na uendelezaji wa rasilimali ya jotoardhi kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati (anayeshughulikia Nishati Jadidifu), Dkt. Khatibu Kazungu.
Mhandisi Luoga amesema kuwa Kongamano hilo la Uendelezaji Jotoardhi Afrika linafanyika kwa mara ya pili nchini Tanzania ambapo kwa mara ya kwanza kongamano la Tano lilifanyikia jijini Arusha mnamo mwaka 2014.
"Kongamano hili linafanyika kwa siku saba (7) kuanzia tarehe 21 hadi 27, tarehe 21 hadi 22 ni siku ambazo yanatolewa mafunzo mbalimbali kuhusu jotoardhi, mafunzo hayo yanatolewa na wabobezi kutoka vyuo mbalimbali vikiwemo vya Tanzania, New Zealand na Japan ambapo wataalam wataelezea masuala ya sayansi, sheria, sera na kanuni zinazosimamia uendelezaji wa jotoardhi," alisema Mhandisi Luoga.
"Katika siku hizo mbili, wataalam watachakata namna ya kuendeleza jotoardhi katika maeneo ya kiufundi, sera, uwekezaji na fedha." Alimalizia Mhandisi Luoga.
Kongamano hilo litafunguliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango Oktoba 23, 2024 na litafungwa Oktoba 25, 2024 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa.
Kongamano hilo linalotarajiwa kuwa na washiriki zaidi ya 800 linahusisha Mawaziri husika kutoka nchi 13 za bara la Afrika zilizopitiwa na bonde la ufa, vile vile kuna nchi nje ya bara hilo ambazo huwa zinashirikiana na Tanzania katika uendelezaji wa jotoardhi zikiwemo za Japan, New Zealand na Iceland nazo zitashiriki.