Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Washirika wa Maendeleo Waombwa Kushirikiana na Serikali Kutatua Changamoto za Kiuchumi
Aug 01, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Farida Ramadhan - WFM, Zanzibar

Serikali imewahimiza washirika wa maendeleo kushiriki katika kuwezesha nchi kufufua fursa zote za kiuchumi zilizozuiwa na kuharibiwa na athari za Uviko- 19 pamoja na vita inayoendelea baina ya Urusi na Ukraini.

Wito huo umetolewa na Makamu wa kwanza wa Rais, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman wakati akifungua Mkutano wa Majadiliano ya Kimkakati kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo uliofanyika katika Hotel ya Seaclif, Zanzibar.

Alisema Serikali inatambua michango mbalimbali iliyotolewa na washirika hao lakini bado inahitaji ushirikiano wao katika kuiwezesha nchi kufikia malengo yake.

Wote tunajua uchumi wa Dunia kwa mwaka 2022, umetikiswa na vita baina ya Urusi na Ukraini, hii imetokea katika kipindi ambacho nchi nyingi duniani zilikua zimeanza kuimarika kutoka katika janga la UVIKO - 19, Tanzania Bara na Zanzibar pia ni miongoni mwa nchi zilizoathirika kwa kuwa inategemea wawekezaji na ushirikiano wa wadau wa maendeleo”, alisema Mhe. Othman Masoud Othman.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Salim Mkuya alisema pamoja na mambo mengine, mkutano huo utajadili namna ya kuiwezesha nchi kutumia rasilimali zilizopo kwa ajili ya kukuza uchumi.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango ambaye ni Mwenyekiti wa Mkutano huo, Bw. Emmanuel Tutuba aliwataka washirika wa maendeleo kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutekeleza sera mbalimbali za kiuchumi kwa maendeleo endelevu.

Alisema Serikali inatambua na kuthamini michango yao kwa kuwa anaamini mafanikio na maendeleo ya uchumi yanategemea michango yao na matokeo ya majadiliano hayo yataiwezesha nchi kufikia malengo yake ya ukuaji uchumi.

Alisema mada zinazojadiliwa katika mkutano huo wa siku mbili ni pamoja na uchumi wa taifa kwa ujumla na masuala ya mazingira kwa kuangalia changamoto ya kimazingira na tabia ya nchi.

Kwa upande wake Mwenyekiti Mwenza wa Washirika wa Maendeleo nchini, Bw. Zlatan Milisic alisema washirika wa maendeleo wataendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika majadiliano yanayohamasisha uwazi na uawajibikaji kwa maendeleo ya Watanzania.

Aliipongeza Serikali kwa kufanikisha zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ambalo matokeo yake yatatumika kwa maendeleo ya kiuchumi.

Alisema washirika wa maendeleo pia wanaipongeza Serikali kwa kuwa na uongozi bora unaozingatia haki za binadamu pamoja na jitihada mbalimbali ilizozichukua kuboresha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi