Na Mwandishi Wetu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alipoingia madarakani,baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ni dhahiri kuwa walio wengi hawakumwelewa hasa anataka nini na pia ana dhamira gani katika kuwaletea wananchi maendeleo, pia falsafa yake ya kuwajali wanyonge na kuhakikisha angalau wanaonja matunda ya nchi yao ilionekana ni kama anawachukia walionacho.
Miongoni mwa watu ambao kwa dhati kabisa ama kwa utashi wao wa kisiasa hawakuwa radhi kuona mafanikio yoyote yanayotokana na uongozi wa Rais Magufuli ni badadhi ya wanasiasa hasa wa vyama vya upinzani ambao hadi leo kuna wanaoamini kwamba kila kinachofanywa na Mhe.Rais hakina maslahi wala tija kwa watanzania.
Wanasiasa hawa hawa ambao katika awamu ya nne walilalamika kuwa Rais anasafiri sana, cha kushangaza katika awamu hii waligeuka na kukana kauli na misimamo yao ya awali na kuanza kumlaumu Rais Magufuli kuwa anakaa mno nchini bila kusafiri ili akajifunze kutoka huko. Mbali na safari pia wanasiasa walilalamikia kuwa semina na posho lukuki kwa watumishi na mashirika ya umma kufanyia vikao nje ya nchi sasa havipo tena, kwa hali ya kawaida unaweza kushangaa kuwa hawa watanzania wenzetu wanalijua walitendalo ama la.
Jitihada nyingi zilizofanyika zilionekana kama uonevu kwa baadhi ya watu hata pale walipoambiwa walipe kodi halali ya Serikali pia wanasiasa wetu waliona kama ni uonevu. Nchi hii ilikua haikusanyi kodi ipasavyo ndio maana wanufaika wa kodi ile walikuwa baadhi ya watu, ndio maana serikali ilishindwa kutekeleza miradi yake ya kuhudumia wananchi. Lakini sasa hivi kodi inakusanywa na miradi inaonekana kuzinduliwa kila uchao.
Hoja kuu iliyosukuma kuandikwa kwa makala hii ni hivi karibuni kuona baadhi ya wanasiasa hasa wa upinzani kuwa wameona kazi inayofanyika na kukiri hadharani kuwa mambo sasa yanakwenda tofauti na hapo awali walipokuwa wakibeza na kukejeli kila jambo linalofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli.
Hivi karibuni Mbunge wa Iringa Mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mheshimiwa Mchungaji Peter Msigwa, alitoa pongezi na shukrani za dhati kwa Rais Magufuli kuwa anatekeleza kazi zake bila kubagua vyama wala mikoa kwani ameendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo jimboni kwake.
Akizungumza katika Ikulu ndogo ya Iringa kwenye hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na Rais kwa viongozi wa Mkoa huo, Mchungaji Msigwa alisema: “Mheshimiwa Rais umekuwa ukisisitiza katika hotuba zako kwamba wewe hujali vyama na hili limedhihirika kwa kweli hujali vyama, umesaidia sana na bahati mbaya hawakukupangia ratiba ya kufungua miradi. Hela kutoka kwako zimekuja nyingi”.
Alitaja baadhi miradi iliyotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Magufuli kuwa ni pamoja na barabara ya kiwango cha lami kutoka Mlandege mpaka kwa Mkuu wa Wilaya ya Iringa yenye thamani ya shilingi bilioni 3.5, stendi ya Ipogolo yenye thamani ya shilingi bilioni tatu na mradi wa maji.
“Kuna vitu vimefanyika na kwa kweli Mheshimiwa Rais hupendelei, hela zinakuja na hata sisi ambao ni wa CHADEMA unaleta hela, kwa hiyo wewe huwa hujali vyama na kwa hilo nikupongeze sana”, alisisitiza Mhe. Msigwa.
Ukomavu huu wa kisiasa ulioonyeshwa na Mchungaji Msigwa unapaswa kuigwa na wanasiasa wengine. Pale inapohitajika kupongeza basi wafanye hivyo lakini pia kama kuna jambo la kukosolewa likosolewe kwa hoja na pia wawe na majibu ya kushauri ni namna bora ambayo itaweza kuwa suluhisho.
Ni dhahiri kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inatumia fedha nyingi katika kuimarisha na kujenga miundombinu ya barabara, madaraja, barabara za juu (flyovers), miradi mikubwa ya maji, umeme pamoja na kugharamia utoaji wa elimu bure na mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu. Haya yote ni mafanikio ambayo kama nchi ni lazima kujivunie kwa kuwa ni maendeleo ambayo yanaonekana na yanagusa maisha ya watanzania wengi hasa wale wa hali ya chini.
Kuna mambo mengi makubwa yamefanyika na yanaendelea kufanyika kwa maslahi mapana ya nchi, mfano ununuzi wa ndege mpya pamoja na kulifufua Shirika la Ndege la Tanzania (ATC), kujenga reli ya kisasa (standard gauge railway) ambayo siyo tu itafungua milango ya kiuchumi kwenye mikoa itakayopita na kuongeza mizigo inayoingia na kutoka katika bandari ya Dar es Salaam, bali hata kwa nchi jirani kwani watanufaika na reli hiyo ikizingatiwa nchi hizo hazina bandari.
Mradi wa mtambo wa kufua umeme wa Stieglers Gorge katika maporomoko ya mto Rufiji na Kinyerezi I extention na Kinyerezi II ni miongoni mwa mafanikio ambayo kama hayataonekana kwa sasa hakika vizazi vijavyo vitanufaika na kukumbuka mchango wa uongozi uliotukuka wa Awamu ya Tano.
Dhana ya upinzani sio kukinzana ndio maana hata katika demokrasia zilizokomaa hutakuta mtu anajitoa ufahamu kwa kukejeli jambo ambalo liko wazi na linaonekana dhahiri.
Mmwendelezo wa wapinzani kuendelea kumuelewa Mhe. Rais umeendelea kujidhihirisha mwishoni mwa wiki wakati wa uzinduzi wa daraja la mto Kilombero maarufu kama daraja la Magufuli na barabara ya Ifakara Kidatu.
Wakati wa uzinduzi huo, Mbunge wa Mikumi, Mheshimiwa Joseph Haule maarufu kama ‘Professor Jay’ alimshukuru Rais kwa kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji Mikumi na kumuomba asaidie kukamilika kwa mradi mwingine wa maji katika Kata ya Ruaha ili kuondoa tatizo la maji katika jimbo la Mikumi.
Aidha, kwa kutambua umuhimu wa kushirikiana na Serikali katika kutatua kero za wananchi, Mbunge huyo alimuomba Rais asaidie utekelezaji wa ahadi ya ujenzi wa barabara inayotokea Korogwe kupitia Handeni, Turiani, Dumila, Kilosa, Mikumi, Malinyi mpaka Songea.
Kazi ya Mbunge ni pamoja na kuwawakilisha wananchi wa Jimbo lake katika kutetea maslahi yao, na hapa ‘Profesa Jay’ alionesha ukomavu kwani hakulalamika na kutoa lawama tu, bali alimuomba Rais kusaidia suala la upatikanaji wa mafao kwa baadhi ya waliokuwa wafanyakazi wa kiwanda cha sukari cha Ilovo pamoja na upatikanaji wa fidia kwa wananchi waliochukuliwa maeneo yao wakati wa ujenzi wa barabara kwani taasisi za umma zilizopitiwa na mradi zimeshalipwa fidia.
Kwa upande wake, mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali alimuomba Mhe. Rais awasaidie wananchi wake upatikanaji wa ardhi kwani kumekuwa na wawekezaji ambao wanamiliki mashamba makubwa bila kuyaendeleza huku wananchi wakiwa na shida kubwa ya ardhi.
Katika kuonesha kuwa Rais hana upendeleo bila kujali itikadi za vyama vya siasa, Rais Magufuli aliyashughulikia mambo mengi yaliyoombwa na mengine aliyatolea maamuzi hapo hapo jukwaani.
Kwa kuwa waliokuwa wakibeza maendeleo na miradi mbalimbali mikubwa inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano sasa wameanza kuona walikuwa hawana sababu ya msingi ya kupinga, ni vyema sasa wakajikita katika kuwaletea wananchi wao maendeleo pamoja na kufanya siasa za kistaarabu na zenye tija kwa mustakabali wa ustawi wa wananchi hasa wale wa hali ya chini.
Wakati wapinzani nchini Tanzania wakianza kumuelewa Rais Magufuli, viongozi mbalimbali duniani wao waliishamuelewa Rais Magufuli na Serikali yake.
Rais wa zamani wa Nigeria, Mhe. Olusegun Obasanjo, aliwahi kumsifia Rais Magufuli kwa juhudi anazofanya kuhakikisha uwekezaji na rasilimali za nchi vinakkuwa na manufaa kwa Tanzania.
“Juhudi anazozifanya Rais Magufuli kuhakikisha uwekezaji kutoka nje unainufaisha nchi ni muhimu na zinapaswa kuigwa na viongozi wengine wa Afrika kwa sababu ndio njia pekee itakalolifanya bara la Afrika kuendelea kiuchumi”, alisisitiza Mhe. Obasanjo.
Mwanazuoni na Wakili Maarufu ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Tume ya Kudhibiti Rushwa nchi Kenya, Profesa Patrick Loch Otieno Lumumba, amekuwa akimuelezea Rais Magufuli kama kiongozi wa kipekee barani Afrika kutokanana ujasiri na juhudi za kupambana na rushwa, kutetea rasimali za nchi na kuhakikisha anajenga uchumi.
Lakini hivi karibuni katika Mkutano wa Nne wa kikao cha kwanza cha Bunge la Afrika Mashariki uliofanyika Dodoma, mmoja wa Wabunge wa Bunge hilo Mhe. Namara Dennis, alishindwa kuzuia hisia zake juu ya uongozi wa Rais Magufuli na dhamira yake ya dhati ya kuimarisha uchangamano ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashari.
“As one person said, and I believe it today that, some men are born great, others achieve greatness. Your Excellency, indeed you are born great and achieve greatness”, alieleza Mbunge Namara Dennis akiashiria kuwa Rais Magufuli amezaliwa na uwezo mkubwa na kufanikiwa kwa kiasi kikubwa sana.
Mwisho.