[caption id="attachment_45682" align="aligncenter" width="750"] Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Samson Anga, akifungua semina ya mafunzo ya kuwajengea uwezo wanawake makandarasi wa mikoa ya Kigoma, Tabora, Rukwa na Katavi. Mafunzo hayo yanafanyika katika Chuo cha Veta mkoani Kigoma.[/caption]
Wito umetolewa kwa makandarasi wanawake kwenye mikoa ya Kanda za Magharibi na Nyanda za Juu Kusini kujitokeza na kuchangamkia fursa za miradi midogo inayojitokeza katika utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa mkoani Kigoma.
Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Samson Anga, ametoa wito huo wakati akizungumza kwenye mafunzo ya wiki mbili kwa makandarasi wanawake kutoka mikoa minne ya Kanda ya Magharibi na Nyanda za Juu Kusini kwa ajili ya kuwajengea uwezo ili kushiriki kwenye kazi za ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara hapa nchini.
"Wanawake msilale changamkieni fursa za hii miradi na msing'ang'anie tu kazi hizi za kufyeka nyasi na kuzibua mitaro kwenye madaraja bali mjitokeza hata kwenye kazi za ujenzi wa barabara", amesisitiza Mhe. Anga.
[caption id="attachment_45683" align="aligncenter" width="750"]Aidha, Mkuu wa Wilaya hiyo ameongeza kuwa fursa za utekelezaji wa miradi midogo kwenye miradi mikubwa inayo nafasi kubwa ya kuwajengea uwezo wa kitaalam na kifedha wahandisi wanawake nchini hivyo ni wajibu wao kutumia nafasi hiyo sasa ambapo mkoa wa Kigoma unayo fursa ya utekelezaji wa miradi mingi ya ujenzi ambayo wakandarasi wengi wanaweza kujitokeza na kuifanya.
Mhe. Anga amesema kuwa bado makandarasi wengi wanawake mkoani Kigoma hawajajitokeza kwa wingi kushiriki kwenye miradi ya ujenzi fursa ambayo inawanyima kukua kimtaji na uwezo wa utekelezaji wa kazi na miradi mingi ya ujenzi.
Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa Kigoma, Mhandisi Narcis Choma, amesema kuwa kwa sasa mkoa Kigoma unatekeleza mradi mkubwa wa barabara kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilometa 260 ambapo zipo kazi ambazo wakandarasi hao wanawake wanaweza kuzifanya.
[caption id="attachment_45685" align="aligncenter" width="750"]Mhandisi Choma amesema kuwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Sera ya uwezeshaji wanawake kiuchumi imeweka mkakati wa kuwasaidia na kuwapa kipaumbele kushiriki katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ambayo inatekelezwa chini ya Wizara hiyo.
Awali Mratibu wa Kitengo cha Ushirikishwaji Wanawake katika kazi za barabara kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Gladiness Kitaly, amesema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwapa ujuzi makandarasi hao wanawake kujua namna ya kuomba miradi ya barabara, taratibu za kujaza zabuni za maombi ya miradi, ufanisi wa teknolojia ya nguvu kazi katika kufanya matengenezo ya barabara katika maeneo ambayo yanatoa kipaumbele kwa wanawake.
Mafunzo hayo ya wiki mbili yameshirikisha wahandisi wanawake kutoka katika mikoa ya Katavi, Rukwa, Tabora na wenyeji Kigoma.