Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wanaotenguliwa Kupunguziwa Mishahara
Jun 14, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, akiwasilisha Bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/2023, Bungeni jijini Dodoma. Juni 14, 2022.

Na Lilian Lundo - MAELEZO

Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imependekeza viongozi wanao tenguliwa kwenye nafasi za kuteuliwa kulipwa mishahara yao ya zamani.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba ametoa pendekezo hilo leo, Juni 14, 2022 Bungeni Jijini Dodoma alipokuwa akiwasilisha mapendekezo ya serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2022/23.

"Napendekeza yeyote aliyetoka kwenye nafasi yake ya kuteuliwa, akitolewa akabaki kwenye utumishi wa Umma, arejee pia kwenye mshahara wake wa zamani, ili kuwapunguzi Watanzania mzigo wa kuwalipa watu waliokaa benchi huku wakiziba nafasi za vijana wapya kuajiriwa," alifafanua Dkt. Mwigulu.

Aliendelea kusema kuwa, unaweza kukuta nchi ina wizara 25 ila ina Makatibu Wakuu 50 au zaidi au Halmashauri 184, lakini kuna Wakurugenzi 300 au zaidi na hivyo hivyo kwa nafasi nyingine, ambapo wengine wamesababisha upotevu na hasara kwa Taifa, lakini wanaendelea kulipwa mishahara kwa nafasi walizoteuliwa.

Dkt. Mwigulu amesema kuwa, Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan  anakerwa kuona fedha nyingi zinakwenda kwenye matumizi ya kawaida, hivyo ameshauri viongozi hao wanapotenguliwa walipwe mishahara yao ya zamani ambayo walikuwa wanalipwa kabla ya kuteuliwa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi