Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wanaoingiza Vifaranga vya Kuku Kinyemela Kubanwa
Jul 11, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Mbaraka Kambona, Pwani

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amesema Serikali haitavumilia vitendo vya uingizwaji wa vifaranga vya kuku kwa njia za panya hapa nchini kwa sababu vinasababisha nchi kukosa mapato na kufubaza jitihada za uwekezaji nchini.

Ulega alitoa kauli hiyo wakati wa ziara yake wilayani Kibaha, mkoani Pwani alipotembelea mashamba ya kutotoleshea vifaranga vya kuku ya Organia na Mkuza Chicks aliyoifanya Julai 11, 2022.

 Akizungumza na wawekezaji wa mashamba hayo kwa nyakati tofauti, Waziri Ulega alisema kuwa kuanzia sasa Wataalamu waliopo wilayani na katika mipaka yote ya nchi watakuwa makini kufuatilia kwa karibu na wale wote wanaoingiza vifaranga kiholela na wakabainika watawajibishwa.

"Hawa watu wanaoingiza vifaranga kienyeji bila kufuata sheria, taratibu na kanuni zetu sio tu wanasababisha nchi kukosa mapato bali wanaangusha uwekezaji wa ndani ya nchi na uchumi kwa ujumla", alifafanua.

Ili kukabiliana na vitendo hivyo, Waziri Ulega aliwaelekeza Wataalamu wanaohusika na usimamizi wa vibali vya kuingiza vifaranga kuandaa mfumo madhubuti utakaokuwa na taarifa zitakazowezesha Serikali kujua na kusimamia vizuri zoezi hilo la utoaji vibali. 

"Tunamshukuru sana Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amefanya kazi nzuri sana ya kualika wawekezaji nchini, sasa ni kazi yetu kila mmoja kulinda uwekezaji wa namna hii",alisema

Aidha, alitumia fursa hiyo kuwaomba Wafugaji wa kuku nchini kuziamini kampuni zinazozalisha vifaranga hapa nchini huku akiongeza kuwa kama kuna changamoto yoyote inayotokana na wazalisha hao basi wasisite kuziwasilisha Wizarani ili zifanyiwe kazi kwa lengo la kuboresha huduma hiyo.

"Lakini vilevile tunaponunua vifaranga vya hapa nyumbani inasaidia kukuza uchumi wetu, kuweka usalama wa uwekezaji tunaowaalika kuja kuwekeza hapa nchini," aliongeza

Awali, wawekezaji wa Mkuza Chicks na Organia walimueleza Naibu Waziri huyo kuwa changamoto kubwa wanayokabiliana nayo kwa sasa ni uingizwaji holela wa vifaranga kutoka nje jambo ambalo linasababisha biashara hiyo kutokuwa ya uhakika.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi