Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wananchi Watolewa Hofu Kuchafuka kwa Mto Mara
Mar 26, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO

Kamati ya Wataalamu iliyoundwa na Serikali kuchunguza chanzo cha uchafuzi katika Mto Mara, imewatoa hofu wananchi na kuwataka kuendelea na shughuli zao za kiuchumi na kijamii ambazo ni rafiki kwa mazingira katika eneo hilo.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Prof. Samwel Manyele kutoka Idara ya Uhandisi wa Kemikali na Madini katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam amewatoa hofu wananchi kupitia taarifa aliyotoa leo Jijini Dodoma, ambapo amesema kuwa chanzo kikubwa cha uchafuzi wa mto huo ni tope na si kemikali.

“Kufuatia uchunguzi wa kimaabara uliofanyika kwenye sampuli zilizochukuliwa zilionyesha kwamba, kiasi cha kemikali za sumu kilichomo kwenye sampuli za maji na sampuli za samaki ni kidogo ukilinganisha na viwango vilivyoweka kwa mujibu wa sheria. Pia, vipimo vya papo kwa papo vya sampuli za maji kutoka kwenye ardhi oevu na visima vilivyo karibu na Mto Mara, vilionesha kuwa ubora wa maji hayo ulikuwa katika viwango vinavyotakiwa, hivyo, maji hayo ni salama kwa matumizi ya binadamu”, alisema Prof. Manyele.

Akieleza kuhusu chanzo cha tatizo, Mwenyekiti huyo amesema kwamba mvua kubwa iliyonyesha katika eneo husika ilisababisha tope lililoko chini ya mto ambalo ni zaidi ya mita takriban 10 kutoka juu ya maji hadi kwenye kina litibuke, hivyo kutokana na mvua kutokuendelea kunyesha, mto huo umeshindwa kujisafisha na endapo mvua zingeendelea mto huo ungeweza kujisafisha wenyewe”, alisema Prof. Manyele.

Mwenyekiti huyo amefafanua kuwa tabia ya kujisafisha kwa mito ni jambo la kawaida duniani na hata katika mto huo ilishawahi kutokea, hali hiyo ya weusi wa maji iliyopo inaweza kuendelea kuwepo kwa kipindi fulani hadi hapo mvua zitakapoanza kunyesha.

Prof. Manyele amezitaja sababu zingine za uchafuzi wa mto huo walizozibaini kuwa ni kubadilika kwa rangi ya maji kuwa nyeusi na kutoa harufu mbaya kulikosababishwa na uozo wa mrundikano wa viumbe-vifu vya mimea vilivyopo chini ya maji na vinyesi vya wanyamapori na mifugo pamoja na hali ya utando wa mafuta iliyoonekana juu ya maji ya mto iliyotokana na mchakato wa uozaji wa viumbe-vifu vya mimea iliyopo kwenye eneo oevu la Mto huo ambao ulitibuliwa na mvua kubwa na hivyo kuelea juu ya maji.

Aidha, matumizi makubwa ya Oksijeni wakati wa uozeshwaji wa rundo la viumbe- vifu vilivyo chini ya maji pamoja na wingi wa mimea maji iliyoota kwenye eneo oevu la Mto huo, yalisababisha upungufu wa hewa ya oksijeni katika maji ya Mto na kusababisha vifo vya samaki waliopo katika Mto huo.

Kwa upande mwingine, kamati hiyo imependekeza kuimarisha utekelezaji na uzingatiaji wa Sheria na Kanuni zinazosimamia eneo oevu la Mto Mara na vyanzo vya maji pamoja na kufanya tathmini ya kina katika eneo hilo ili kuona uwezekano wa kulitangaza kuwa eneo lindwa.

Vilevile, kamati imependekeza utafiti zaidi ufanyike katika eneo hilo ili kubaini aina za mimea na wanyama waliopo pamoja na mbinu za kukabiliana na mimea vamizi katika eneo hilo inayotishia kutoweka kwa Mto Mara, kuundwa kwa Programu ya pamoja ya Hifadhi ya Bonde la Mto Mara pamoja na kutengwa kwa maeneo ya kutosha ya malisho nchini ili yaweze kukidhi mahitaji ya mifugo na kuondoa uwezekeno wa mifugo kuvamia maeneo ya ardhi oevu na ya vyanzo vya maji.

Mwanzoni mwa mwezi Februari 2022, iliripotiwa kuwepo kwa mvua kubwa zilizodumu kwa muda mfupi hali iliyopelekea kubadilika kwa rangi ya maji ya Mto Mara na kuwa nyeusi ikiambatana na harufu mbaya pamoja na utando wa mafuta juu ya maji ya mto na kusababisha baadhi ya viumbe kama samaki kufa. Kutokana na tukio hilo, Serikali iliunda Kamati ya wataalamu 11 kutoka taasisi mbalimbali za Serikali kwa ajili ya kuchunguza chanzo cha tukio hilo na kutoa mapendekezo ya kukabiliana na hali hiyo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi