Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wananchi Watakiwa Kulinda Maeneo Yenye Hifadhi za Historia
Aug 13, 2020
Na Msemaji Mkuu

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt.Harrison Mwakyembe akizungumza na uongozi wa Wilaya ya Tunduru, alipokua katika ziara ya kukagua usikivu wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) pamoja na kukagua maeneo ya Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika yaliopo katika shule ya sekondari Masonya ambapo alipata nafasi ya kuzungumza na wanafunzi hao mnamo Agosti 12,2020. Mwenye suti ya kaki kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Bw. Julius Mtatiro na kulia ni Mratibu wa mradi huo, Bw. Boniface Kadili.

Na Shamimu Nyaki –WHUSM,Tunduru

Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amezitaka jamii zinazoishi katika maeneo ambayo yamebeba urithi wa historia na utamaduni wa nchi kuyalinda na kuyatunza maeneo hayo kwa kuwa ni hazina kwa Taifa.

Dkt. Mwakyembe ametoa rai hiyo Agosti 12, 2020 alipotembelea maeneo ya Mradi wa Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika yaliyoko katika shule ya wasichana ya Masonya wilayani Tunduru mkoani Ruvuma ambapo amesema kuwa eneo hilo ni miongoni mwa maeneo ambayo yamebeba historia ya bara la Afrika.

“Ni lazima wananchi wakafahamu umuhimu wa maeneo haya, ni maeneo ambayo yabeba historia ya viongozi wa Afrika akiwemo Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere. Rais wa zamani wa Msumbiji hayati Samora Machel na wengine ambao walipigania uhuru wa bara hili, hivyo ni jukumu la wananchi wanaozunguka maeneo hayo kutambua umuhimu wake ili wayatunze”, alisema Mhe. Mwakyembe.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Mhe. Julius Mtatiro amesema kwamba eneo la Masonya limebeba historia ya ukombozi wa bara la Afrika hivyo ni vizuri eneo hilo likatambulika na kupewa hadhi ya makumbusho ya Taifa.

“Eneo hili ni muhimu sana na lina hadhi ya kuwa eneo la utalii wa kiutamaduni kwa ukanda huu wa nyanda za juu kusini hivyo nchi yetu ikishirikiana na nchi ya Msumbiji kulihifadhi litakuwa ni eneo litakalovutia watalii” alisema Bw.Mtatiro.

Naye Mratibu wa Mradi huo, Bw. Boniface Kadili ameeleza kuwa utafiti wa kubaini maeneo yaliyotumika katika harakati za ukombozi wa bara hili unaendelea kufanyika ambapo mpaka sasa zaidi ya maeneo 200 yamebainishwa na kuwekwa katika kumbukumbu.

Bw. Kadili ameongeza kuwa kwa sasa Serikali inaendelea na utaratibu wa kurasimisha mradi huo ili utambulike kisheria na Tanzania kama Mwenyekiti wa mradi huo iweze kuwa na nguvu ya kisheria ya kuusimamia.

Mradi wa Program ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika una jukumu la kulinda na kuhifadhi historia ya nchi ambazo zilisaidiana katika kujikomboa ikiwemo Malawi,Afrika Kusini,Msumbiji,na nyingine ambazo Tanzania ilikuwa mstari wa mbele kuzisaidia kupata uhuru.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi