Wananchi wa Kilolo, Mkoani Iringa, wanatumia muda mfupi kusafiri na kusafirisha mazao yao, kufuatia kukamilika kwa ujenzi wa Barabara ya Kidabaga - Boma la ng'ombe, yenye urefu wa km 18.3 iliyojengwa kwa kiwango cha lami.
Kukamilika kwa barabara hiyo ni utekelezaji wa malengo ya serikali ya awamu ya sita, ambayo kupitia Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA), inalenga kuhakikisha kuwa barabara za Vijijini zinaboreshwa ili kuwezesha wananchi, kusafiri, kusafirisha mazao yao kwa urahisi na kukuza uchumi wao.
Mwenyekiti wa Bodi ya TARURA, Mhandisi Florian Kabaka, ameeleza kufurahia kukamilika kwa ujenzi wa Barabara hiyo kwakuwa umeenda kwa wakati na kwamba sasa unatoa nafasi kwa wakala wake, kuendelea na kazi nyingine ya kuwaondolea wananchi adha, kufuatia mradi wa Barabara za “Agri-Connect,’’ unaotekelezwa katika mikoa mwili ukiwemo Iringa, chini ya ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Jumuiya ya Ulaya (EU).
“Ni jukumu la bodi kuzisimamia barabara hizo na kumuunga mkono Rais Samia, ambaye ameamua kwa dhati kuhakikisha kuwa barabara za Vijijini zinafunguka na kuwafikia wananchi ili ziwaunganishe na miji na kurahisisha usafiri na usafirishaji, lengo kubwa likiwa pamoja na mambo mengine, kukuza kipato chao kiuchumi'', alikazia Mhandisi Kabaka.