Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wananchi 57,638 Wapata Chanjo ya Uviko-19 Rukwa - Dkt. Kasululu
Jan 20, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na OMM Rukwa

Wananchi wa Mkoa wa Rukwa wamepongezwa kwa kujitokeza kupata chanjo ya kinga dhidi ya ugonjwa wa UVIKO - 19 ambapo hadi kufikia mwezi Januari mwaka huu watu 57,638 wamefanikiwa kupata chanjo hiyo katika vituo vya afya.

Akizungumza kwenye kikao cha Umoja wa Machifu wa mkoa huo jana (19.01.2022) mjini Sumbawanga, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Dkt. Boniface Kasululu alisema tangu zoezi hilo la kutoa dozi za chanjo lilipoanza mwezi Julai 2021 kumekuwa   na mwitikio mzuri toka kwa wananchi.

Mganga Mkuu huyo alieleza mafanikio ya chanjo kwa wananchi yaliyopatikana ni pamoja na kupungua kwa watu waliolazwa kwa maambukizi ya UVIKO - 19 pia kutokuwepo taarifa za watu waliopata madhara baada ya kupata dozi ya chanjo ya UVIKO-19.

“Kwa kupitia chanjo ya kinga dhidi ya UVIKO-19 hatusikii tena kusongamana kwa wagonjwa wodini hata vifo vimepungua kwenye mkoa wetu.

Rukwa tulipokea dozi 68,683 za chanjo ya UVIKO-19 ambapo watu 57,638 sawa na asilimia 84 tayari wamechanjwa”, alieleza Dkt. Kasululu.

Kwa upande wake Chifu Kiongozi wa Machifu, Mkoa wa Rukwa na Mkuu wa Mkoa Mstaafu, Joachim Wangabo aliwasihi Machifu kwenda kuelimisha na kuhamasisha jamii hususan Wazee kujitokeza kupata chanjo.

Chifu Wangabo alisema yeye binafsi tayari amechanja pia atarudia kupata dozi ya pili ya chanjo ili kukamilisha kwa mujibu wa utaratibu wa wataalam na kuongeza kuwa Serikali imelenga kuwafanya wananchi wake wawe salama na wenye kinga dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19.

Akizungumza kwenye kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joseph Mkirikiti aliwataka viongozi hao wa Machifu kufundisha maadili mema kwa jamii ili amani na maendeleo kwa mkoa yaendelee kupatikana kwani viongozi hao wanaheshimika vizuri kwenye jamii.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi