Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wananchi 15,823 Wanufaika na Mradi wa Maji Liuli, Nyasa
Jan 09, 2024
Wananchi 15,823 Wanufaika na Mradi wa Maji Liuli, Nyasa
Muonekano wa tenko la maji lililopo Liuli wilayani Nyasa
Na Lilian Lundo – MAELEZO

Wananchi 15,823 wa Kata ya Liuli waliopo Vijiji vya Nkalachi, Liuli, Hongi, Mkali A na Mkali B wamenufaika na mradi wa maji wa Liuli wilayani Nyasa, na kuondokana na adha ya kutumia muda mwingi kutafuta maji badala ya kufanya shughuli za maendeleo.

Meneja wa RUWASA Wilaya ya Nyasa, Bw. Masoud Samila amesema hayo wakati wa mahojiano na Maalum na Maafisa wa Idara ya Habari - MAELEZO mwishoni mwa mwezi Desemba, 2023 wilayani humo.

“Hali ya utekelezaji wa mradi kwa ujumla umefikia wastani wa asilimia 95. Tunaishukuru Serikali kwa kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa mradi huu ambao utasaidia kupunguza kero ya maji kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kumtua ndoo mama kichwani,” amesema Bw. Samila.

Amesema mradi huo unaogharimu shilingi bilioni 4.7 bila Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), unatekelezwa kwa fedha za Mfuko wa Maji wa Taifa (NWF) na Fedha za Serikali Kuu (GoT), chini ya Mkandarasi Mzawa Emirates Company Limited.

Aidha amesema kuwa, mradi huo wa maji unahusisha ujenzi wa chanzo cha maji (Intake) ambao umefikia asilimia 98, ulazaji wa bomba kuu lenye urefu wa mita 12782 umekamilika kwa asilimia 99, ujenzi wa matanki matatu yenye ujazo wa lita 135,000, lita 100,000 na lita 300,000 umekamilika kwa asilimia 98 pamoja na ujenzi wa vituo 19 vya kuchotea maji (DPs) ambao umekamilika kwa asilimia 95.

Wakiongea kwa nyakati tofauti wananchi wanaofaidika na mradi huo wa maji wameipongeza Serikali kwa kuwapelekea mradi huo maji, kwani kwa muda mrefu walikuwa wakipoteza muda mwingi kutafuta maji badala ya kufanya shughuli za kujiongezea kipato.

“Zamani tulikuwa tunapata shida ya maji, tunamshukuru Mungu ametujalia Rais mwenye kujua watu wake wana shida ya maji. Kijiji chetu kimepata bomba la maji, ambayo yanatoka kwa saa 24. Hivyo kwa sasa tumeondokana na kero ya kutopata maji katika kijiji chetu cha Liuli” amesema Bi. Ziada Wami mkazi wa Kijiji cha Liuli.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Liuli, Petro Mkwera amesema, “Hapo awali kabla ya ujio wa mradi huu, maji yalikuwa yanapatikana kwa shida hasa kipindi cha kiangazi. Wakina mama walikuwa wanatumia muda mwingi kutafuta huduma ya maji. Kutokana na ukosefu wa maji safi na salama kulisababisha magonjwa ya mlipuko kijijini hapa. Baada ya kuja huu mradi, kweli faraja ipo, watu wanapata maji, na yanapatikana muda wote”.

Mwenyekiti huyo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwakomboa wanakijiji wa Liuli, hususan wakina mama ambao wamekuwa wakitumia muda mwingi kutafuta maji badala ya kufanya shughuli za kuwaingizia kipato.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi