Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wanahabari Wamiminika Karimjee Kupata Chanjo ya UVIKO 19
Aug 12, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Na John Mapepele, WHUSM


Wanahabari, Wanamichezo na Wasanii wameendelea kumiminika leo, Agosti 12, 2021 katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya zoezi la hiari la kupata chanjo ya UVIKO 19.

Zoezi hili limeratibiwa na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Wizara ya Afya. 


Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi, alifafanua kwamba makundi hayo yamependekezwa kupewa kipaumbele na Serikali kwa kuzingatia, pamoja na mambo mengine, umuhimu wao kwa jamii na ukweli kwamba kwa mazingira ya kazi zao, wako katika hatari ya kuambukizwa.


“Zoezi hili ni la siku mbili Agosti 12-13, 2021, litafanyika katika Ukumbi wa Karimjee Jijini Dar es Salaam kuanzia saa tatu asubuhi, natoa wito kwa wadau wote kwa hiari yao watumie fursa hii iliyotolewa na Serikali ili wajikinge na wawakinge wengine na UVIKO-19” ameongeza Dkt. Abbasi.

Dkt. Abbasi ameendelea kuwasihi wale waliokosa kujiandikisha awali wawe Wasanii, Wanahabari au Wanamichezo waendelee kuwasiliana kupitia namba 0654063274 au barua pepe matiko.mniko@basata.go.tz  ya Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA). 


Amesisitiza kuwa Wasanii walio nje ya Dar es Salaam wataendelea kutumia utaratibu unaoendelea kutangazwa na Wizara ya Afya.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi