Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wanafunzi Watakiwa Kuwa na Maadili Mema: Jaji Mkuu
Oct 18, 2018
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_36972" align="aligncenter" width="750"] Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akisalimiana na waalimu wa Shule ya Sekondari Nyampulukano iliyopo wilayani Sengerema alipofika ili kuzungumza na wanafunzi wa shule hiyo kuhusu masuala ya maadili.[/caption]

Na Lydia Churi- Sengerema Mwanza

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka wanafunzi  kuwa na maadili mema, kufuata sheria na taratibu za nchi na kuachana na matendo yote yanayokiuka maadili ikiwemo wizi wa mitihani.

Akizungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari ya Nyampulukano iliyopo wilayani Sengerema mkoani Mwanza, Jaji Mkuu aliwaambia wanafunzi hao kuwa wizi wa mitihani ni tatizo la kwanza la ukosefu wa maadili katika jamii.

Aliwataka wanafunzi hao kujenge tabia ya kujisomea mambo mbalimbali kwa kuwa karne hii ya ishirini na moja ni karne ya sayansi na teknolojia yenye taarifa nyingi zitakazowasaidia kwa maendeleo yao.

“Karne hii ya ishirini na moja ni tofauti na karne ya ishirini, someni mambo mbalimbali ili mfahamu nchi yenu inakwendaje”, alisema Jaji Mkuu huku akiwasisitiza waisome Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025 ili wafahamu  Tanzania itakuwa ni nchi ya namna gani.

[caption id="attachment_36973" align="aligncenter" width="750"] Wanafunzi wa kidato cha tano na cha sita wa shule ya sekondari nyampulukano iliyopo Sengerema wakimsikiliza Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.[/caption]

Aidha, Jaji Mkuu pia aliwashauri wanafunzi watakaopenda kuwa wanasheria hapo baadaye kuhakikisha wanakuwa waadilifu katika jamii kwa kuwa fani ya sheria inahitaji mtu aliye na maadili mema hasa na yule anayechukia na kuvipinga kwa nguvu zote vitendo vya rushwa.

Hata hivyo alisema kutokusoma sheria hakutawazuia kufahamu sheria mbalimbali za nchi na kuwa karne hii ya ishirini na moja inahitaji fani zote kushirikiana ili kuwa na maendeleo.

Akizungumzia rushwa na uchumi wa nchi, Jaji Mkuu alisema ziko nchi duniani zenye rasilimali nyingi na zimeweza kubadili maisha ya raia wake na wakati huo huo zipo nchi zenye rasilimali nyingi lakini hazijaweza kubadili maisha ya watu wake kutokana na rushwa hivyo aliwataka wanafunzi hao kukataa rushwa kwa kuwa ni adui wa maendeleo yao.

Mahakama ya Tanzania imeanzisha mpango wa kuzitembelea shule mbalimbali nchini kwa lengo la kuwaandaa vijana kuwa na maadili mema katika jamii wakiwamo wanasheria wa baadaye.

Jaji Mkuu anaendelea na ziara yake ya kikazi katika mkoa wa Mwanza ambapo anakagua shughuli za mahakama kwenye Mahakama zilizopo mkoani humo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi