Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wanadiplomasia Waahidi Kuendelea Kushirikiana na Tanzania Kuvutia Wawekezaji Zaidi
Jan 22, 2021
Na Msemaji Mkuu

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo  akieleza jambo kwa Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania Mhe. Manfred Fanti wakati  walipokutana na kufanya mazungumzo kuhusu masuala ya uwekezaji  leo Januari 22,2021 Jijini Dodoma.

Na Mwandishi wetu- Dodoma

Umoja wa Ulaya umeahidi kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Tanzania katika jitihada za kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini ikiwa ni pamoja na kuvutia wawekezaji wengi zaidi kutoka nchi za Umoja wa Ulaya kuja kuwekeza hapa nchini.

 Hayo yamesemwa leo, Januari 22, 2021 Jijini Dodoma na Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania Mhe.Manfred Fanti alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo  akiwa kwenye picha ya pamoja na Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania Mhe. Manfred Fanti mara baada ya kukutana na kufanya mazungumzo kuhusu masuala ya uwekezaji  leo Januari 22,2021 Jijini Dodoma.

“Nimekuwa nikisikia ushuhuda kutoka kwa wawekezaji wengi wanaotoka nchi za Umoja wa Ulaya kuwa wanapata faida katika uwekezaji wao hapa nchini na nikiwa kama mwakilishi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania ni jukumu langu kuhakikisha kuwa nashirikiana ipasavyo na Serikali ya Tanzania kuvutia wawekezaji wengi zaidi kuwekeza Tanzania”, alisema Mheshimiwa Balozi Fanti.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo (kulia)  akisisitiza jambo kwa  Naibu Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania Bibi Lianne Houben ambapo katika mazungumzo hayo walijadili na kukubaliana maeneo mbalimbali yanayoweza kuboreshwa ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi kutoka nchini  Uholanzi.

Aliongeza kuwa, Umoja wa Ulaya unatambua jitihada zinazoendelea kufanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika kuboresha mifumo ya kisheria, kisera na ya kitaasisi ili kuweka mazingira rafiki zaidi yatakayovutia wawekezaji na hivyo wako tayari kuendelea kuiunga mkono Serikali ili kufanikisha lengo hilo.

Katika mazungumzo hayo, Waziri Kitila Mkumbo na Balozi Fanti walijadili pia maeneo bayana  ambayo Tanzania na Umoja wa Ulaya wanaweza kukuza ushirikiano wa uwekezaji  ikiwemo katika sekta ya uzalishaji nguo, uchimbaji na uchakataji wa madini, uchakataji wa mazao ya mifugo na uvuvi, uzalishaji wa nishati.

Vilevile Waziri Mkumbo aligusia baadhi ya maeneo ya kimkakati ambayo tayari Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeweka nguvu kuyatekeleza ikiwemo kuandaa na kutekeleza  Mkakati wa Taifa wa Uwekezaji, utekelezaji wa programu ya kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara (ROADMAP) pamoja na kuandaa mfumo kabambe wa ukusanyaji takwimu za uwekezaji nchini.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo (kushoto)  akipokea kitabu kinachoeleza masuala mbalimbali kuhusu nchi ya Uholanzi kutoka kwa Naibu Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania Bibi Lianne Houben mara baada ya mazungumzo yao leo Jijini Dodoma kuhusu masuala ya uwekezaji.

Aidha, Alimweleza Balozi huyo kuwa hayo ni baadhi ya maeneo ambayo Serikali ipo tayari kuendelea kushirikiana na Umoja wa Ulaya, ili pamoja na mambo mengine, kumaliza kabisa changamoto zinazowakabili wawekezaji wa kigeni hapa nchini.

Kwa upande mwingine Waziri huyo wa Uwekezaji alikutana pia na Bibi Lianne Houben, Naibu Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania ambapo katika mazungumzo hayo walijadili na kukubaliana maeneo mbalimbali yanayoweza kuboreshwa ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi, hususani wanaotoka nchi ya Uholanzi. Baadhi ya maeneo hayo ni pamoja na kuweka mfumo mzuri wa kuziwezesha Taasisi mbalimbali Wezeshi zinazohudhumia wawekezaji kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi huku zikizingatia maslahi mapana ya wawekezaji, pamoja na suala la uhaba wa wafanyakazi wenye ujuzi na fani mbalimbali ambazo wawekezaji wanazihitaji.

Uholanzi ni moja ya nchi zinazoongoza kwa kuwa na wawekezaji wengi nchini Tanzania waliowekeza katika sekta za mbalimbali kama vile Kilimo (kwa mfano makampuni ya maua yaliyowekeza Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro), huduma za kifedha (kwa mfano Benki ya NMB), Viwanda (kwa mfano Kampuni Unilever na Heineken), usafirishaji (kwa mfano Kampuni ya KLM), nk. Takwimu zinaonesha kuwa takribani miradi 161 ya kutoka Uholanzi  imesajiliwa katika za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ikiwa na mitaji yenye jumla ya thamani ya Dola za Marekani biilioni 1.1 na kutoa ajira 13,995.

Naibu Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania Bibi Lianne Houben  akisisitiza jambo kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo leo Januari 22,2021 Jijini Dodoma  wakati wa mazungumzo yao  kuhusu masuala ya uwekezaji.

(Picha na MAELEZO)

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi