Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Walimu Wanaodai Watakiwa Kuwasilisha Vielelezo kwa Maofisa Elimu.
Jan 10, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na Tiganya Vincent - RS Tabora

WALIMU wenye madeni halali mkoani Tabora wametakiwa kuhakikisha wanawasilisha vielelezo vinavyoonyesha uhalali wa madai yao kwa Maofisa Elimu waliopo karibu nao ili yaweze kufanyiwa kazi mapema.

Kauli hiyo ilitolewa jana wilayani Igunga na Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Tabora anayeshughulikia Elimu, Suzan Nussu wakati akiongea na walimu wa Shule ya Sekondari ya Ziba alipokuwa ameongozana na Mkuu wa Mkoa huo  Aggrey Mwanri ili kukagua ujenzi wa mabweni ya wanafunzi.

Alisema kuwa ni vema zoezi hilo likafanyika mapema na kwa makini ili walimu wanaodai madai ya haki waweze kupata fedha zao kama alivyoagiza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli hivi karibuni.

“Nawaomba walimu wenzangu mhakikishe mnawaeleza wenzenu wenye madeni kupeleka madai yao mapema kwa Maofisa Elimu waliokaribu nao ili nao waweze kuyawasilisha mapema Mkoani kwa ajili ya hatua zaidi, ucheleweshaji wowote unaweza kuwasababisha walimu wachelewe pia kupata haki yao” alisisitiza Nussu.

Aidha Katibu Tawala huyo Msaidizi wa Mkoa aliwaonya walimu na Maofisa Elimu kutofanya udanganyifu wowote kwani fedha kidogo inaweza ikawasababisha wapoteze kazi zao na hata kujikuta katika vyombo vya Sheria.

Alisema kuwa walimu wanapopeleka madai yao ni vema wakajiridhisha kuwa ni kweli wanadai na madai yao ni kweli ili kujiweka katika mazingira salama.

Nussu aliongeza kuwa Maofisa Elimu katika Halmashauri zote za Mkoa wa Tabora ni vema wakahakikishe walimu wote wanapata taarifa ili waweze kufikisha taarifa hizo haraka mkoani.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi