Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wakulima wa Usagali AMCOS Wamuomba RC Kuwasaidia Walipwe Deni Lao.
Jan 19, 2018
Na Msemaji Mkuu

 Na Tiganya Vincent - Rs Tabora

Wakulima wa Tumbaku wa Chama cha Msingi cha Ushirika Usagali (AMCOS) wilayani Nzega wameiomba Serikali ya Mkoa wa Tabora kuwasaidia kusimamia madai yao ya fedha kiasi cha shilingi milioni 193 za mauzo ya tumbaku kwa msimu 2015/2016 huku wakilaumu kuwa fedha hizo zilichukuliwa na viongozi waliokuwa madarakani wakati huo.

Wakulima hao walitoa kilio hicho jana katika Kijiji cha Usagali wilayani Nzega wakati Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri akiwa katika ziara ya kutembelea Vyama vya Ushirika kuhimiza upandaji miti kupitia ushirika kwa ajili ya kurudisha uoto wa asili na kukifanya kilimo cha tumbaku kiwe rafiki kwa mazingira.

Mmoja wa wakulima, Peter Mashoto alisema kuwa waliokuwa Viongozi wa Usagali na wajumbe wa Bodi wanatuhumiwa kulipwa fedha na Kampuni ya Tanzania Leaf Tobacco Company (TLTC) lakini wao walishindwa kuwalipa wakulima waliouza tumbaku yao na kuzichukua wao kwa ajili ya matumizi binafsi.

Aliongeza kuwa wakulima waliodhurumiwa fedha hizo wameendelea kuishi maisha ya dhiki wakati watuhumiwa wanaendelea kuishi maisha mazuri na kujiendeleza wao binafsi huku wao wakishinda hata kuwaendeleza watoto wao kielimu.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa sasa wa Usagali AMCOS, Alphonce Sylvester aliomba Mrajisi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora kuwasaidia kusimamia madai ya wakulima ili waweze kulipa fedha zao na kuwarudishia matumaini.

Sylvester aliongeza kuwa ili kurudisha matumaini kwa wakulima ni vema Serikali isaidie kusimamia ili haki itolewe na wakulima waweze kupata fedha zao.

Kufuatia kilio hicho cha wakulima hao, Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mwanri aliwaagiza viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega kwa kushirikiana na Ofisi ya Mrajisiri Mkoa kufuatilia suala hilo na kuona limekwamia wapi ili wakulima waweze kupatiwa haki yao kama madai yao ni halali.

Aliongeza kuwa ni jukumu lao kuhakikisha wanawashika mkono wakulima waliodhurumiwa ili hatua dhidi ya wahusika zichukuliwe kwa ajili ya kuhakikisha haki inatendeka.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Nzega, Jacob Ntalitinya aliahidi kushirikiana na viongozi wa Ushirika kushughulikia tatizo hilo ili wakulima wapate fedha zao na wahusika wachukuliwe hatua zinazostahili.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi