Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wakulima wa Tumbaku na Mbaazi Kuwa na Soko la Uhakika
Nov 17, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na Beatrice Lyimo-MAELEZO, DODOMA

Serikali imeendelea kutafuta masoko ya mazao ya Biashara ikiwemo tumbaku na Mbaazi kwa kuzungumza na wafanyabiashara wa mazao hayo ili kuwawezesha Wakulima kuwa na soko la uhakika.

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa tisa wa bunge la Jamhuri la Muungano wa Tanzania Bungeni mjini Dodoma.

“Tumefanikiwa kuyapata Makampuni mawili ya TGTS na Alliance One ambayo yako tayari kununua tumbaku iliyobaki kuanzia jumanne wiki ijayo na kwa sasa wanaratibu vituo vya tumbaku ilipo ili wakachukue” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Mhe. Majaliwa ameongeza kuwa, kumekuwa na malalamiko ya wakulima juu ya tatizo la masoko ya mazao ya tumbaku na mbaazi nchini ambapo suala la mbaazi Serikali inawasiliana na Serikali ya India ili ikikubali kununua mbaazi zote.

Aidha amesema kuwa Serikali imechukua hatua mbalimbali za kuimarisha sekta ya kilimo ikiwa ni pamoja na kuratibu maandalizi, pembejeo(mbegu na madawa), kuimarisha ushirikiano, masoko na kuimarisha Bodi za Mazao, pale palipo na Bodi.

Wakati huo huo Mhe. Majaliwa amesema kuwa, juhudi za utangazaji utalii zimesaidia ongezeko la watalii kutoka 1, 137,182 mwaka 2015 hadi kufikia 1, 284,279 mwaka 2016 sawa na asilimia 12.9.

Aidha amesema kuwa, Serikali ina mpango wa kuendeleza utalii Nyanda za Juu Kusini ambako kuna vivutio vingi vya utalii lakini pamekuwa na idadi ndogo ya watalii wanaotembelea ukanda huo ukilinganisha na ukanda wa Kaskazini.

“ Katika kutekeleza hilo, Serikali imepokea Dola za Marekani milioni 150 kupitia mradi wa Resilient Resource for Tourisim and Growth kwa ajili ya kutekelezwa kuanzia mwaka wa fedha 2017/2018 ambapo lengo la mradi huo ni kuongeza mchango wa sekta ya utalii katika uchumi kwa kuongeza ubora wa vivutio vya utalii kwa kuboresha miundombinu ndani ya hifadhi, usimamizi wa maliasili na kuongeza faida kiuchumi” amefafanua Waziri Mkuu Majaliwa.

Mbali na hayo, Waziri Mkuu amemuagiza Waziri wa Maliasili na Utalii kuanzisha Mamlaka ya Fukwe za Bahari na Maziwa ili kutangaza na kuendeleza fukwe ambazo hazina shughuli.

Akizungumzia hali ya uchumi nchini, Waziri Mkuu amesema kuwa, viashiria muhimu vya uchumi jumla vinaonesha kwamba mwenendo wa uchumi ni wa kuridhisha.

“Kufuatia kuongezeka kwa makusanyo ya kodi na usimamizi thabiti wa matumizi ya Serikali, nakisi ya bajeti ya Serikali imeshuka na kufika Asilimia 1.9 kwa mwaka 2016/2017” ameongeza Waziri Mkuu Majaliwa.

Hata hivyo amesema kuwa, Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu viashiria vya uchumi jumla ili kuwezesha hali bora ya maisha ya wananchi walio wengi hasa vijijini.

Waziri Mkuu Majaliwa amehairisha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hadi Januari 30, mwaka 2018.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi