Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wakazi wa Magu Watakiwa Kuacha Kujichukulia Sheria Mkononi
Aug 16, 2023
Wakazi wa Magu Watakiwa Kuacha Kujichukulia Sheria Mkononi
Mkuu wa Wilaya ya Magu Rachel Kassanda akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata ya Bujashi akiwa katika ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo iliyopo Wilaya ya Magu
Na Yusuph Digossi Afisa Habari Magu

Mkuu wa Wilaya ya Magu, Rachel Kassanda amewataka wakazi wa wilaya hiyo kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi pindi wanapowakamata wahalifu na badala yake washirikiane na vyombo vya ulinzi na usalama kwa ajili ya kuwachukulia hatua za kisheria wahalifu wanaokamatwa.

DC Kassanda ametoa agizo hilo jana Jumatano Agosti 16, 2023 wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata ya Bujashi akiwa katika ziara yake ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo iliyopo Wilaya ya Magu pamoja na kuzungumza na kusikiliza kero za wananchi.

Akizungumza na wananchi wa Bujashi, DC Kassanda amewaasa wakazi wa Kata hiyo kuacha tabia hiyo mara moja kwani ni kinyume cha sheria na taratibu za nchi kwa sasabu vyombo vya ulinzi na usalama vipo kwa ajili ya kutatua changamoto hiyo, hivyo wananchi wanapokamata mhalifu wanatakiwa kutoa taarifa katika mamlaka husika ili hatua zichukuliwe.

Aidha, amewahimiza wananchi wa Magu kulinda na kuthamini miradi ya maendeleo iliyopo wilayani humo ili iendelee kunufaisha wananchi na kuunga mkono juhudi za serikali kutoa huduma bora kwa wananchi.

Katika hatua nyingine, DC Kassanda amewataka wazazi kuendelea kusimamia suala la maadili ya watoto haswa kukemea tabia ya utoro shuleni kwa watoto.

Kuhusu changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi hao, DC Kassanda amewataka wananchi kuziwashilisha kwa viongozi wao kuanzia ngazi ya Kata ili uongozi wa wilaya uzifanyie kazi.

DC Kassanda anaendelea na ziara ya kukagua shughuli za miradi ya maendeleo ambapo anatarajia kutembelea kata 25 za Wilaya ya Magu kuanzia tarehe 16-25/08/2023.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi