Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wakandarasi Walioshindwa Kukamilisha Miradi Ya REA II Kuchukuliwa Hatua.
Dec 22, 2017
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_25475" align="aligncenter" width="750"] Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akizungumza na wakandarasi wanaotekeleza miradi ya usambazaji wa umeme vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) katika mkoa wa Tanga, watendaji kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijiji (REA) hawapo pichani.[/caption]

Na Greyson Mwase.

Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amesema kuwa wakandarasi walioshindwa kukamilisha miradi ya usambazaji wa umeme vijijini Awamu ya Pili (REA II) watachukuliwa hatua za kisheria na Serikali.

Mgalu ameyasema hayo leo katika ofisi za Wizara ya Nishati zilizopo jijini Dar es Salaam katika kikao chake na wakandarasi wanaotekeleza miradi ya usambazaji wa umeme vijijini Awamu ya Tatu katika mkoa wa Tanga inayosimamiwa na  Wakala wa Nishati Vijijini.

Wakandarasi hao ni pamoja na kampuni ya Derm inayosambaza miundombinu ya umeme katika  wilaya za Handeni, Kilindi, Korogwe na Lushoto,  Kampuni za Radi, Njarita na Aguila zinazosambaza umeme katika  wilaya za Mkinga, Pangani, Muheza na Bumbuli na kampuni ya Namis Cooperate Ltd inayosambaza miundombinu ya umeme katika wilaya zote za Tanga.

Kikao hicho pia kilishirikisha watendaji kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA)

[caption id="attachment_25476" align="aligncenter" width="750"] Wakandarasi wanaotekeleza miradi ya usambazaji wa umeme vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) katika mkoa wa Tanga, watendaji kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) wakifuatilia maelekezo yaliyokuwa yanatolewa na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (hayupo pichani)[/caption]

 

Naibu Waziri Mgalu, alisema kuwa wakandarasi waliopewa kazi ya kusambaza miundombinu ya kusambaza umeme vijijini kupitia REA Awamu ya Pili walilipwa malipo karibia yote hivyo walipaswa kukamilisha miradi yote kwa wakati.

Aidha, aliwataka wakandarasi wanaotekeleza miradi ya REA Awamu ya Tatu kuongeza kasi katika miradi ya usambazaji wa umeme vijijini na kuongeza kuwa kipaumbele kitolewe katika taasisi kama Shule, Vituo vya Afya, zahanati, Visima vya Maji ili wananchi waanze kufurahia  huduma za jamii.

Vilevile aliwataka wakandarasi wanaotekeleza miradi ya REA katika mikoa miwili tofauti kuhakikisha kuwa kasi inakwenda kwa kiwango sawa na kuepuka kuwekeza nguvu kwenye mkoa mmoja tu.

“Kwa wakandarasi wanaosambaza miundombinu ya umeme katika mkoa zaidi ya mmoja lazima wahakikishe kasi inakwenda sawa kwa mikoa yote, pasiwepo na mkoa ambao mradi wake unakamilika mapema huku mkoa mwingine ukiwa nyuma kabisa,” alisisitiza Mgalu.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Mgalu alitoa tahadhari kwa wakandarasi watakaobainika wanaingiza nguzo za umeme na tranfsoma nje ya nchi tofauti na maelekezo yaliyotolewa awali kuwa vifaa vyote vya ujenzi wa mradi wa umeme vitoke hapa nchini.

Alisema Serikali ilishakutana na wadau wa vifaa ikiwamo wasambazaji wa Nguzo za Umeme na kiwanda cha kutengeneza Transfoma cha TANALEC kilichopo jijini Arusha na kujiridhisha uwezo wa wadau hao katika usambazaji wa vifaa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi