Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wahasibu, Wagavi na Watunza Hazina Mikoa ya Lindi na Mtwara Wanufaika na Mafunzo ya Epicor 10.2
Jun 04, 2018
Na Msemaji Mkuu

Katibu Tawala wa mkoa wa Mtwara, Alfred Luwanda akifungua mafunzo ya mfumo wa Epicor 10.2  kwa wahasibu, maafisa ugavi na  waweka hazina jana mjini Mtwara.

Na  Mwandishi  Wetu

MAFUNZO yenye lengo la kuondoa changamoto za utoaji wa taarifa hasa kutoka kwenye vituo vya kutolea huduma pamoja na kuunganisha taarifa hizo kwenye Hesabu za Halmashauri yanayofanyika kikanda nchini kote yameanza jana.

Mafunzo hayo yanayozingatia mfumo wa Epicor toleo la 10.2 utakavyobadilishana taarifa na mfumo wa kuandaa mipango na bajeti (PlanRep) pamoja na mfumo wa taarifa za fedha katika ngazi ya kituo cha kutolea huduma (FFARS) yanashirikisha Waweka Hazina, Maafisa Usimamizi Fedha wa Mikoa, na Wahasibu.

Mfumo huo pia hutoa taarifa za utekelezaji za mipango na bajeti kwa kuzingatia matumizi ya fedha yaliyofanyika.

Akifungua mafunzo hayo katika Kanda ya Kusini, Katibu Tawala wa mkoa wa Mtwara, Alfred Luanda alisema matumizi ya mfumo wa Epicor toleo la 10.2 ni hatua kubwa katika utekelezaji wa dhana nzima ya uwazi, uwajibikaji na utawala bora katika usimamizi wa Fedha za umma.

 Mkuu wa Timu ya  fedha  kutoka mradi wa Kuboresha Mifumo ya sekta za umma (PS3) Dkt. Gemini Mtei akizungumzia umuhimu wa mafunzo ya mfumo wa Epicor 10.2 mjini Mtwara jana.

“Hii ni nafasi ya pekee ya kupata mafunzo ya mfumo wa usimamizi wa fedha za umma wa Epicor toleo la 10.2 ambao umeboreshwa ili kuweza kubadilishana taarifa na  mfumo wa Mipango na Bajeti wa PlanRep na ule wa uhasibu na kutoa taarifa za fedha za vituo vya kutoa huduma, FFARS,” alisema Luanda.

Katika mafunzo hayo ya yaliyoanza jana (04 june) katika kanda sita nchini, Luanda aliwataka washiriki kuhakikisha wanapata elimu yote inayofanikisha mifumo ya LGRCIS (Mfumo wa Mapato), PlanRep, FFARS na Epicor kuweza kubadilishana taarifa.

Mafunzo hayo yaliyofadhiliwa na Serikali ya Marekani, kupitia mradi wa Uimarishaji Mifumo ya Sekta za Umma (PS3) unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID), yanafanyika katika kanda sita nchini kote, ikiwamo mkoani Mtwara.

Aidha Luanda alisema tangu mradi huu umeanza kutekelezwa, taifa limeshuhudia mafanikio katika utendaji kazi katika Mikoa na Halmashauri kutokana na mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kuendelea kuimarishwa na kuwapo na upatikanaji wa taarifa sahihi, na kwa wakati huku Makatibu Tawala wa Mikoa ambao ni viongozi wa Mikoa kuweza kuona matumizi  na mapato kupitia  mifumo ya TEHAMA.

Afisa kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Bw. James Bukumbi akiwasilisha mada kuhusu mfumo wa Epicor  10.2 leo mjini Mtwara wakati wa mafunzo kwa wahasibu, maafisa ugavi na waweka hazina  jana mjini Mtwara.

Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Bw. James Bukumbi  akiteta jambo na Mkuu wa Timu ya Mifumo ya Fedha PS3 Dkt. Gemini Mtei  wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi wa kada za uhasibu na waweka hazina wa Halmashauri za Mikoa ya Lindi na Mtwara.

Mafunzo haya ya mfumo wa Epicor toleo la 10.2 yanalenga kuwapa uelewa wa mabadiliko na maboresho yaliyofanyika katika mfumo. Hatua mbalimbali zimepitiwa katika historia ya Mfumo wa Epicor, kama Platinum toleo la mwaka 1999/2000 na Epicor 7.2 mwaka 2001 toleo ambalo lilifungwa katika Halmashauri 38.

Mnamo mwaka 2004/05 toleo la 7.2 liliboreshwa kwenda toleo la 7.3.5 na kufungwa katika Halmashauri 44 zaidi na kufanya jumla ya Halmashauri 82 zilizokuwa zinatumia mfumo wakati huo.

Sehemu ya washiriki wa mafunzo ya mfumo wa Epicor 10.2 kutoka mikoa ya Mtwara na  Lindi yanayofanyika mjini Mtwara yakiwashirikisha  wahasibu, maafisa ugavi na waweka hazina jana mjini Mtwara.

(Picha zote na Ps3)

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi