Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wahasibu na Watunza Hazina Wanufaika na Mafunzo ya Mfumo wa Usimamizi wa Fedha ( Epicor 10.2)
Jun 08, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na: Nashon Kenedy

 WAHASIBU na watunza hazina kutoka mikoa ya Kagera na Kigoma wameipongeza Serikali kupitia Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa kuwawezesha kupata mafunzo maalum ya mfumo wa usimamizi wa fedha, ambayo yanalenga kuleta ufanisi sehemu za kazi.

Wakizungumza katika mahojiano maalum na gazeti hili mjini Bukoba jana, watumishi hao wamesema wanaishukuru serikali na wafadhili kwa pamoja kwa kuwajengea uwezo katika eneo hilo muhimu la kimfumo, ambapo awali walikuwa wakifanya majukumu yao kwa uelewa ambao ulihitaji mafunzo zaidi.

Akizungumza kwa furaha, Mhasibu Msaidizi kutoka Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera Vedastina Gaspary alisema mafunzo hayo ambayo yametolewa kwa muda mfupi yatamuwezesha katika utekelezaji wa majukumu yake ya kiutendaji katika mfumo wa Epicor na upelekaji wa fedha moja kwa moja kwenye vituo vya kutolea huduma (FFARS).

“ Mafunzo haya siku nne, kutokana na umuhimu wake, yalistahili yawe ya siku kumi, walimu wametufundisha vizuri mpaka tumefahamu, na tumefanya majaribio kwa vigtendo namna ya uendeshaji wa mfumo wa epicor ingawa kulikuwa na tatizo la kimtandao”, alisema.

Kwa upande wake, Afisa Msimamizi wa Fedha Mwandamizi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Pius Ngaiza alisema mafunzo hayo yamempatia manufaa makubwa kwa kupata uelewa namna mfumo wa epicor 10.2 unavyofanya kazi.

Alisema kupitia mafunzo hayo amegundua kuwa mfumo wa Epicor 10.2 utakavyoanza kufanya kazi utaondoa tatizo la uandaaji wa taarifa hasa utofauti wa takwimu kutokana na mifumo ya fedha kuanza kubadilishana taarifa.

“ Kwa uelewa niliopata nitasimamia halmashauri katika mkoa wangu  na kuwafundisha kwa uhakika pale watakapokuwa wamekwama kuutumia mfumo huu wa epicor 10.2, na nawashukuru wafadhili Mradi wa PS3 kwa kutuletea mafunzo haya muhimu kwa ajili ya kuleta ufanisi kwenye utendaji wa kazi zetu”, alisema.

Baadhi ya washiriki wengine walisema kuwa mafunzo hayo yamewawezesha kupiga hatua muhimu kwa kwenda kuleta mabadiliko sehemu za kazi kwa madai kuwa awali walikuwa wakitoa taarifa kwenye mfumo mmoja na kuzipeleka kwenye mfumo mwingine, tofauti na sasa ambapo walisema mifumo hiyo itakuwa ikifanya kazi yenyewe.

Mfumo wa Epicor 10.2 umeandaliwa mahususi kuungana na mifumo mingine kwa lengo la kukidhi matakwa ya maboresho yanayoendelea na yaliyopo nchini na kuwajengea uwezo watumishi wa halmashauri na mikoa waweze kutumia mfumo huo kwa kutoa huduma bora za kiutendaji kwa wananchi.

MWISHO

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi