Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wahamasishwa Kutumia Nishati Safi za Kupikia 
Sep 04, 2024
Wahamasishwa Kutumia Nishati Safi za Kupikia 
Mhandisi wa Miradi kutoka REA, Kelvin Tarimo akiwasilisha mada ya nishati safi ya kupikia kwa wanawake zaidi ya 650 katika Mkutano Mkuu wa kwanza wa Mtandao wa Wanawake wa Jeshi la Magereza uliofanyika Septemba 04, 2024 jijini Dodoma
Na Mohamed Seif - REA

Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea kuhamasisha wananchi kutumia Nishati Safi za Kupikia kwa lengo la kuwezesha utunzaji wa mazingira, kuboresha afya na ustawi wa jamii sambamba na kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

 

Mhandisi wa Miradi kutoka REA, Kelvin Tarimo amesema hayo hivi leo Septemba 04, 2024 jijini Dodoma alipokuwa akiwasilisha mada ya nishati safi ya kupikia kwa wanawake zaidi ya 650 katika Mkutano Mkuu wa kwanza wa Mtandao wa Wanawake wa Jeshi la Magereza.

 

“Matumizi ya nishati safi za kupikia ni ajenda inayolenga kukabiliana na ongezeko la uharibifu wa mazingira pamoja na athari za kimabadiliko ya tabianchi pamoja na athari za kiafya zinazotokana na matumizi ya nishati zisiyo safi za kupikia,” amesema Mhandisi Tarimo.

 

Alifafanua kuwa matumizi ya nishati zisizo safi na salama za kupikia huchangia uharibifu wa mazingira ambapo alibainisha kuwa inakadiriwa zaidi ya hekari zipatazo laki nne za misitu hukatwa kila mwaka kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kibinadamu ikiwemo matumizi ya kuni na mkaa jambo ambalo alisema limekua likisababisha madhara mbalimbali ya kimazingira ikiwemo uharibifu wa vyanzo vya maji na ikolojia kwa ujumla.

 

Mhandisi Tarimo alisema katika kukabiliana na hali hiyo, Wakala kama moja ya mdau mkuu wa masuala ya nishati vijijini itaendelea kuhakikisha inatimiza vyema lengo kuu la utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia 2024-2034 ambao umelenga hadi kufikia mwaka 2034 asilimia 80 ya wananchi wawe wanatumia nishati safi za kupikia. 

 

Amesema REA imejipanga kuhakikisha adhma hiyo inafikiwa kikamilifu kwa kuwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati safi ya kupikia na amewasisitiza wananchi hususan wanawake kuendelea kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo kwenye mnyororo mzima wa thamani wa masuala ya nishati safi ya kupikia.

 

“Hatua tunazoendelea nazo sasa ni pamoja na kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi za kupikia; kuhakikisha upatikanaji wa Nishati Safi, nafuu, endelevu na za uhakika za kupikia kote nchini haswa maeneo ya vijijini na kuhamasisha uwekezaji katika sekta ndogo ya nishati safi ya kupikia,” amefafanua Mhandisi Tarimo.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi