Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wagonjwa Wenye Matatizo ya Moyo Washauriwa Kuhudhuria Kliniki  Bila Kukosa
May 15, 2020
Na Msemaji Mkuu

Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam

 Wagonjwa wenye matatizo ya moyo, kisukari, shinikizo la juu la damu, figo na  saratani wameshauriwa kuhudhuria kliniki zao bila kukosa kwa kufanya hivyo wataweza kuepuka kupata madhara ya kiafya  ikiwa ni pamoja na kupoteza maisha.

Rai hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi  wakati akizungumza kuhusu  kupungua kwa idadi ya wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo tangu virusi vinavyosababisha maambukizi ya ugonjwa wa Corona (COVID -19)  ulipoingia hapa nchini.

Prof. Janabi alisema  hivi sasa idadi ya wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo imepungua kutoka 300 kwa siku  hadi kufikia 50 kwa siku na wagonjwa wanaolazwa idadi yao kupungua  kutoka 150  kwa siku hadi kufikia 30. Kwa upande wa wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji mkubwa wa kusimamisha moyo idadi yao imepungua   kutoka wagonjwa wanne kwa siku na kufikia mgonjwa mmoja . Wagonjwa wanaofanyiwa  upasuaji wa bila kufungua kifua  kupitia tundu dogo wamepungua  kutoka kumi kwa siku na kufikia  watatu.

Mkurugenzi huyo Mtendaji alisema wao kama madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo hawaelewi hivi sasa wagonjwa hao ambao hawahudhurii kliniki wanatibiwa wapi kwani kama mgonjwa ataogopa kwenda Hospitali kwa kuhofia kupata maambukizi ya  ugonjwa wa Corona ambao ukiupata na kupona haukuachi na madhara yoyote na kuacha kliniki za magonjwa ambayo kama usipotibiwa yatakusababishia  madhara makubwa katika mwili wako.

Alisema wagonjwa wa moyo wanatakiwa kuondoa hofu kutokana na taarifa mbalimbali wanazozipata kuhusiana na ugonjwa wa Corona jambo la muhimu wafuate maelekezo ya wataalamu wa afya kwa kufanya hivyo wataweza kuepuka kupata maambikizi ya ugonjwa huo na siyo kuacha  kuhudhuria kliniki.

 “Wote tunafahamu kuwa kutokana na tafiti mbalimbali zilizofanyika Ulimwenguni zinaonesha wagonjwa wenye matatizo ya moyo, kisukari, shinikizo la juu la damu, figo, saratani na watu wenye umri mkubwa wa zaidi ya miaka 60 ndiyo wanaoathirika zaidi na ugonjwa wa Corona ikiwa  wagonjwa hawa hawatahudhuria kliniki  kama walivyopangiwa na madaktari wao wakipata maambukizi ya Virusi vya Corona  ni rahisi kwao kupoteza maisha,” .

“Wagonjwa wa moyo, kisukari, shinikizo la juu la damu, figo na  saratani  kama hawatahudhuria kliniki kwa kuhofia kupata maambukizi ya Virusi vya ugonjwa wa Corona  wanaweza kupata madhara ya kupoteza uhai, kupata  kiharusi, kupoteza baadhi ya viongo vya mwili kwa mfano mguu, kupofuka macho na kupoteza nguvu za kiume  lakini ukipata maambukizi ya Virusi vya  Corona na ukapona hutaweza kupata  madhara yoyote,” alisisitiza Prof.Janabi .

Prof. Janabi alisema ni muhimu wagonjwa hao kwenda Hospitali kutibiwa kwa kuwa mgonjwa akiwa na  magonjwa hayo hawezi kujitibia  nyumbani jambo la muhimu ni kufuata ushauri wa wataalamu wa afya hii ikiwa ni pamoja na kuvaa barakoa, kunawa mikono kwa maji safi yanayotiririka na sabuni, kukaa umbali wa zaidi ya mita moja kati ya mtu na mtu na kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima.

“Taasisi yetu inatuma ujumbe wa  kuwakumbusha wagonjwa wetu kuhudhuria kliniki zao kutokana na tarehe walizopangiwa na madaktari lakini wengi wao hawaji kutibiwa. Ninaendelea kuwasisitiza waje kutibiwa kwani tumechukua tahadhari  zote za kuhakikisha hawapati maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Corona wawapo katika eneo la Hospitali”,.

“Wagonjwa wanaofika kutibiwa hapa wanapimwa joto la mwili kabla ya kuanza kupata huduma ya matibabu, tumefunga mabomba ya maji pamoja na kuweka vitakasa mikono katika maeneo mbalimbali ya Taasisi yetu hii inawafanya kupata nafasi ya kunawa mikono mara kwa mara pia wanakaa umbali wa mita moja kati ya mgonjwa mmoja na mwingine,” alisema Prof. Janabi.

Alisema kuna baadhi ya wagonjwa walipokelewa katika Taasisi hiyo wakiwa na dalili za ugonjwa wa moyo ambazo ni kushindwa kupumua, kukohoa na kuchoka lakini baada ya kufanyiwa vipimo walikutwa na maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Corona na kupelekwa katika vituo vya kuwatibu wagonjwa hao ambako wataalamu wetu wanakwenda kuwapatia matibabu ya moyo.

Kwa upande wao baadhi ya wagonjwa wanaotibiwa katika Taasisi hiyo walisema tangu ugonjwa wa Corona ulipotangazwa hapa nchini wanahudhuria kliniki kama walivyopangiwa na madaktari wao na wanapata huduma walizokuwa wanazipata  kipindi ambacho hakukuwa na ugonjwa huo.

“Nimeanza kutibiwa na wataalamu wa Taasisi hii tangu mwaka 2008 na idadi ya wagonjwa ambao tunahudhuria hapa huwa ni kubwa   ila leo nashangaa idadi ya wagonjwa ni wachache tofauti na siku za nyuma. Kama wagonjwa hawaji Hospitali kwa kuhofia kupata ugonjwa wa  Corona wasifanye hivyo waje kliniki wasiwe na hofu tarehe ya kliniki ikifika waje kwani kuna wakati unaandikiwa vipimo sasa kama hauji kwa daktari vipimo utachukuliwaje?”, aliuliza  Mama Fitina Mkere mkazi wa Kigogo.

Naye Mzee Ali Masukuzi mkazi wa Bagamoyo ambaye anatibiwa katika Taasisi hiyo tangu mwaka 2017 alisema anahudhuria kliniki kila mwezi na hawezi kukosa kliniki kwani  hana hofu na ugonjwa wa Corona kwakuwa  anafuata ushauri unaotolewa na wataalamu wa afya.

“Mimi nachukua tahadhari zote zinazotolewa na wataalamu wa afya hata nikifika hapa Hospitali ninanawa mikono, ninavaa barakoa pia  tunakaa umbali wa mita moja kati ya mgonjwa mmoja na mwingine na nikiwa hapa ninapata  elimu kuhusiana na ugonjwa wa Corona,”.

“Ninawaomba watalamu wa afya wazidi kutoa elimu kwa wananchi hasa wanaosumbuliwa na magonjwa makubwa yakiwemo ya moyo ili wafahamu madhara ya kutokuhudhuria kliniki hasa kipindi hiki cha ugonjwa wa Corona,” alisema Mzee Masukuzi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi