Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wagonjwa wa Moyo 28,876 Wametibiwa Katika Hospitali ya JKCI kwa Kipindi cha Mwezi Julai Hadi Septemba Mwaka Huu
Oct 09, 2019
Na Msemaji Mkuu

Na Mwandishi  wetu

Jumla ya wagonjwa 28,876 wenye matatizo ya moyo wametibiwa kwa kipindi cha miezi mitatu ya Julai hadi Septemba  mwaka huu katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).

Hayo yamesemwa jana na Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Magonjwa ya Moyo Dkt. Peter Kisenge wakati akieleza  taarifa ya kazi zilizofanywa na Kurugenzi yake  katika kikao cha menejimenti kilichofanyika jana katika Taasisi hiyo.

Dkt. Kisenge ambaye pia ni daktari bingwa wa magonjwa ya moyo alisema wagonjwa waliotibiwa katika Taasisi hiyo  wanaume walikuwa 12,566 na wanawake 16,310 ambapo 6,590 sawa na asilimia 22.8 walikuwa wagonjwa wapya.

“Tumeona wagonjwa kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani pamoja na nchi za  Ethiopia, Malawi, Zimbabwe, Visiwa vya Comoro na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Wagonjwa waliotibiwa na kurudi nyumbani walikuwa 27,882 na wagonjwa 994 walilazwa kati ya hao  500 ni wanawake na 494 ni wanaume idadi ya vifo vikiwa ni asilimia 6”, alisema Dkt. Kisenge.

Dkt. Kisenge aliendelea kusema  kuwa watoto waliotibiwa katika Taasisi hiyo walikuwa 1,516 ambapo wa kike walikuwa 800 na wavulana  716 kati ya hao wagonjwa 374 walikuwa wapya.

Dkt. Kisenge alisema, “Wagonjwa wengi tuliowaona walikuwa na matatizo ya shinikizo la juu la damu, kutanuka kwa moyo,valvu, matundu, mishipa ya damu ya moyo  na magonjwa ya moyo ya kuambukizwa yanayosababisha makovu katika  valvu za moyo kutokana na kupata mafindofindo kwenye tezi za koo (Rheumatic Heart disease) ”,.

Wagonjwa waliofanyiwa upasuaji wa bila kufungua kifua na kuzibuliwa mishipa ya damu ya moyo pamoja na kuwekewa vifaa vinavyousaidia moyo kufanya kazi  vizuri  walikuwa 352 kati ya hao watoto 87 sawa na asilimia 24.7 na hakukuwa na mgonjwa aliyepoteza maisha.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Upasuaji Dkt. Anjela Muhozya alisema  wamefanya  upasuaji kwa wagonjwa 153   kati ya hawa wagonjwa 122 walifanyiwa upasuaji wa moyo wa kufungua kifua, wagonjwa 23 walifanyiwa upasuaji wa mishipa ya damu na nane walifanyiwa upasuaji wa mapafu.

“Tumefanya upasuaji wa kubadilisha valvu kwa wagonjwa ambao valvu zao zilikuwa na shida, kurekebisha mishipa ya damu ya moyo na kupandikiza mishipa ya damu ya moyo (Coronary Artery Bypass Graft – CABG). Wagonjwa waliopoteza maisha ni watatu sawa na asilimia 2.5”, alisema Dkt. Anjela.

Dkt. Anjela alisema changamoto kubwa wanayokutana nayo katika matibabu ya wagonjwa wa moyo ni wagonjwa wengi kufika katika Taasisi hiyo huku mioyo yao ikiwa imechoka. Na kuwaomba wagonjwa kujenga tabia ya kupima afya zao mara kwa mara ili kujuwa kama wanamatatizo ya moyo au la na kama watakuwa nayo waweze kupata matibabu kwa wakati.

Naye Cecilia Nthala kutoka nchini Malawi ambaye mtoto wake anatibiwa katika Taasisi hiyo alishukuru kwa huduma ya matibabu ya moyo aliyoipata .

“Nilipata taarifa  ya Taasisi hii kupitia tovuti na mitandao ya kijamii, kwa kuwa mtoto wangu ana matatizo  ya moyo nikawa nafuatilia kwa ukaribu huduma mbalimbali  wanazozitoa baada ya kuridhika nazo  nikaamua kumleta mwanangu ili naye apate huduma ya matibabu”, alisema Cecilia.

“Kwa kipekee ninawashukuru wauguzi na madaktari kwani muda wote wako karibu na mimi najiona kama vile niko nchini kwetu Malawi. Ninawaomba muendelee kutoa huduma kama hii mliyoitoa kwangu kwa wagonjwa wengine mnaowatibu”, alishukuru Cecilia.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi