Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wagonjwa 64 Wahamishiwa Mloganzila
Jan 05, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na Judith Mhina.

Jumla ya wagonjwa 178 kutoka mikoa ya Dar Es Salaam, Pwani na Morogoro wamehamishiwa katika Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi, Kampasi ya Mloganzila (MAMC) hadi kufikia Desemba 31 mwaka jana.

Akithibitisha zoezi hilo, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili – MUHAS Profesa Apolinary Kamuhabwa amesema leo ofisini kwake kuwa kati ya hao 91 ni wanaume na 87 ni wanawake.

Amesema, hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt, John Pombe Magufuli alilolitoa wakati wa uzinduzi wa Hospitali hiyo mwishoni mwa mwaka jana, ambapo walilazwa na kupatiwa huduma katika kitengo cha magonjwa ya ndani.

Profesa Kamuhabwa ameeleza kwamba kati ya wagonjwa 178 waliohamishwa 91 ni wanaume na 87 wanawake. Aidha, Hospitali ya  Taifa ya Muhimbili imepeleka jumla ya wagonjwa 64 na wengine (114) wametoka hospitali za Pwani na Morogoro na wachache ambao wanakwenda wenyewe.

Kaimu Makamu Mkuu huyo ameeleza kuwa, mpaka sasa Vitengo viwili vya magonjwa ya dharura na watoto vimeanza kutoa huduma za upasuaji (Surgical services), magonjwa ya kinamama na uzazi. "Tunatarajia kupokea wagonjwa zaidi kadiri siku zinavyoongezeka”. Amesisitiza.

Kuhusu suala la Watumishi ambalo Rais Magufuli aliagiza litafutiwe ufumbuzi, Prof. Kamuhabwa amesema hadi sasa jumla ya Watumishi wapya 227 wameajiriwa. Kati ya hao 80 ni Wauguzi, 20 ni madaktari wa kawaida na wahudumu wa afya 25 wameripoti kazini tarehe 1 Disemba mwaka jana.

Amesema, hii inafanya idadi ya Watumishi kufikia 762 ikiwa ni pamoja na Watumishi 478 waliokuwepo awali, 114 watumishi wa ajira mpya, 135 wa uhamisho kutoka hospitali mbalimbali  na 229 watumishi wa  MUHAS ambao ni Wahadhiri.

Akiongelea suala la Madaktari wabobezi na bingwa amesema; “Hospitali ina jumla ya madaktari bingwa 33, madaktari wa kawaida 29 na wauguzi 233. Hata hivyo, bado Watumishi zaidi wanahitajika, hasa Wauguzi na Madaktari bingwa ili kuweza kujitosheleza katika vitengo vyote vya Hospitali.

Wakati huo huo, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo - Huduma za Hospitali Profesa Said Aboud amesema MUHAS inafanya mazungumzo na  Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ili kujenga kiwanda cha kutengeneza maji ya drip (Infusion Manufacturing Plant) yanayotumika katika kutolea huduma za matibabu katika Hospitali.

Amesema, Kamati ya watu Watano (5) imeundwa kuandaa Andiko la Mradi kwa ajili ya kuomba ufadhili  kutoka  NHIF kwa ajili ya mradi huu. Andiko ili linatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu wa Januari 2018.

Akielezea kuhusu dawa zinazopatikana hospitalini hapo, Profesa Aboud amesema hivi sasa zipo aina 515 za dawa kati ya 728, sawa na asilimia 70.7 ya dawa zote zinazohitajika. Aina 213 ya dawa zilizosalia zinatarajiwa kupokelewa kutoka Bohari Kuu ya Madawa (MSD) kuanzia mwezi huu wa Januari 2018.  Aidha, MUHAS tayari imeandaa bajeti ya ununuzi wa madawa kwa ajili ya MAMC kwa mwaka huu wa 2018 ili itumwe Wizara ya Afya mwezi huu wa Januari 2018 kama alivyoagiza Rais.

Hospitali ya Mloganzila MAMC imepewa hadhi ya Hospitali ya Taifa ya Rufaa yenye uwezo wa kutoa huduma za afya zinazohitaji madaktari bingwa specialized na madaktari bingwa wabobezi super specialized.

Pia, hospitali imewekwa vifaa tiba vya hali ya juu na vyenye hadhi ya teknolojia ya kisasa, ambapo ina vipimo mbalimbali kama; kipimo cha mawimbi sumaku (MRI), cha CT Scan” cha kuvunja mawe ya figo bila upasuaji (Extracorporeal shock-wave lithotripsy), cha kuchunguza saratani ya matiti (Mammogram),  cha moyo (- ECHO Echgraphy), cha umeme wa moyo (Electrocardiography), cha umeme wa misuli ( Electromygraphy) cha ufanyaji kazi wa mapafu na vifaa vingine vingi vitakavyowezesha utoaji huduma za kiwango cha kimataifa. 

Vifaa hivyo muhimu pamoja na uwepo wa madaktari wabobezi na bingwa katika fani mbalimbali za afya vimeifanya hospitali ya Taaluma na Tiba iwe na uwezo wa kutoa huduma nyeti, adimu ya matibabu na uchunguzi wa wagonjwa hapa nchini.

Hongera Serikali kwa kupunguza kwa kiasi kikubwa gharama zinazotumika kuwapeleka wagonjwa nje ya nchi kwa ajili ya matibabu.  Shime Watanzania wenzangu tuchangamkie fursa iliyopo kuhakikisha tunakwenda hospitali kuchunguza afya zetu na kutambuliwa matatizo yetu ya kiafya na mara upatapo rufaa usisite kufika Mloganzila kwa tiba na matibabu.    

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi