Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wagonjwa 15 Kupata Matibabu ya Kuzibua Mishipa ya Damu ya Moyo
Apr 23, 2019
Na Msemaji Mkuu

Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na mwenzao wa  Hospitali ya Meditrina ya nchini India wanafanya kambi maalum ya matibabu ya moyo kwa  siku tatu ya kuzibua mishipa ya damu  ambayo imeziba kwa kiwango kikubwa (Chronic Total Occlusion) na hivyo kushindwa kupitisha damu vizuri.

Kambi hiyo ni maalum kwa ajili ya  kuwasaidia wagonjwa wenye matatizo hayo ambao bila ya kupata mtaalamu mwenye ujuzi wa hali ya juu wa kuzibua mishipa hiyo wangefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo.

Matibabu hayo yanafanyika kwa kutumia mtambo wa Cathlab ambapo mgonjwa anatobolewa tundu dogo katika paja ambalo linapitishwa vifaa maalum vya kuzibua mishipa ya damu ya moyo (Stent).

Katika kambi hiyo wataalamu wa afya wa JKCI watapata elimu ya jinsi ya kuzibua mishipa ya damu ya moyo ambayo imeziba kwa kiwango kikubwa.

Jumla ya wagonjwa 15 ambao mishipa yao ya damu mmoja hadi mitatu imeziba wanatarajiwa kutibiwa  katika kambi hiyo iliyoanza leo tarehe 23 hadi 25/4/2019. Hadi sasa wagonjwa watano wameshatibiwa na hali zao zinaendelea vizuri.

Imetolewa na:

Anna Nkinda

Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi