Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wafanyabiashara wa Wanyamapori  Hai Waiomba Serikali  Iwasaidie
Jan 11, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na Mwandishi Wetu.

Chama cha wasafirishaji wanyamapori hai nje ya nchi kibiashara (TWEA)   kimeiomba serikali isitishe zuio la kusafirisha nje wanyamapori hao ili wanachama wake waweze kujikwamua na hali ngumu ya maisha inayaowakabili.

Wakizungumza mbele ya  Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga   kwenye kikao  cha Wizara na wawakilishi wa wafanyabiashara hao waliiomba serikali isikilize  kilio chao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama hicho, Enock  Balilemwa alisema baadhi ya wanachama wakiwemo walemavu waliokuwa wamechukua mikopo   benki wamefukuzwa kwenye nyumba zao baada ya kushindwa kufanya marejesho ya mikopo hiyo kufuatia zuio la biashara hiyo.

Alieleza kuwa baadhi ya wanachama wake  wamejikuta kwenye hali ngumu ya kupoteza mali zao na kuingia kwenye mifarakano na wateja wao kwa vile  wafanyabiashara hao walichukua pesa toka kwa wateja kama  malipo ya awali hivyo wakati wa zoezi la kusimamisha biashara linafanyika liliwakuta wafanyabiashara hao wameshachukua pesa za wateja wao kama malipo ya awali.

Naye, Makamu Mwenyekiti wa TWEA, Fatuma Hamis alimweleza Naibu Waziri kuwa  zuio hilo lilifanywa ghafla mno bila kutoa muda kwa wafanyabiashara hao ukizingatia kuwa walikuwa wakimiliki leseni halali walizokuwa wamezilipia pesa bila kuzifanyia kazi ya kuwaingizia kipato.

Aidha,  alimweleza Naibu Waziri huyo kuwa zuio hilo limepelekea wafanyabiashara hao kupoteza uaminifu kwa wateja wao na kuwaweka kwenye mazingira magumu ya ushindani kibishara kwani biashara hiyo haifanywi na Tanzania pekee.

Wakati akijibu hoja za Wafanyabiashara hao,  Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga amekihakikishia  Chama cha Wasafirishaji  Wanyamapori Hai nje ya nchi kibiashara (TWEA) kuyafanyia kazi malalamiko yao kadri itakavyowezekana na kuja na kauli moja ya Serikali.

Amesema lengo la Serikali la kuzuia usafirishaji wanyamapori hao lilikuja baada ya wafanyabishara ambao sio waaminifu kukengeuka kwa kuanza kujihusisha na ujangili pamoja na kusafirisha wanyamapori ambao hawamo kwenye orodha ya vibali walivyopewa.

“Dhumuni la serikali la kusitisha biashara hii  ilikuwa ni  njema tu baada ya kuona wajanja wachache wananufaika huku wanyonge wakibaki watazamaji kwenye rasilimali zao’’ alisema Hasunga.

Hata hivyo, Naibu Waziri Hasunga  alisema lengo la Serikali halikulenga  kuwakomoa bali ni kutaka kuweka mfumo mzuri utakaomsaidia kila  Mtanzania aone ananufaika na rasilimali za nchi yake.

“Nimewasikiliza kwa umakini wa hali ya juu lakini hata hivyo Serikali ina utaratibu wake wa kutoa majibu, tupeni muda ili tukitoa majibu kuhusu hoja zenu kuwe na jibu moja kwa kila mmoja wetu’’ aliongeza Hasunga.

Katika hatua nyingine, Hasunga aliwataka wafanyabishara hao wasisite kuonana nae  muda wowote ule kwa kumpigia simu au kwa kuonana nae pindi wanapokuwa na jambo la kutaka kuzungumza nae kwa ajili ya manufaa mapana ya Wizara na nchi kwa ujumla.

Naye, Kaimu Mkurugenzi  wa Idara ya wanyamapori, Dkt. Nebbo Mwina aliwahakikishia wafanyabiashara kufanyia kazi malalamiko yao kutokana na   hoja za msingi  zilizowasilishwa na wafanyabiashara hao.

“Nimesikia baadhi ya malalamiko yenu ambayo kwa nafasi yangu niliyo nayo kwa kushirikiana na watumishi walio chini yangu, nitayashughulikia” alisema Dkt. Nebbo.

 

 

 

 

 

 

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi