Na. Haika Mamuya na Eva Ngowi, WFM, Dodoma
Serikali imezitaka Wizara, Idara zinazojitegemea na Taasisi za Serikali zinazokusanya mapato yasiyo ya kodi, kuongeza juhudi katika ukusanyaji wa mapato ili kufikia malengo ambayo Serikali imejiwekea kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Rai hiyo imetolewa jijini Dodoma na Kamishna wa Sera wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Elijah Mwandumbya, wakati wa Semina ya taratibu za ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi iliyowakutanisha Maafisa mipango, TEHAMA, Wahasibu na Wakaguzi wa Ndani.
Bw. Mwandumbya alisema tathmini za hivi karibuni zinaonesha mwenendo usioridhisha wa mapato yasiyo ya kodi kwa Wizara, Idara zinazojitegemea na Taasisi za Serikali zinazokusanya mapato hayo ukilinganisha na mapato ya kodi.
“Katika Bajeti ya mwaka huu, Serikali imejipanga kutumia Shilingi trilioni 41, hivyo ni lazima tuikusanye ili kuweza kutekeleza Bajeti iliyopitishwa na Bunge, mapato hayo ni ya kodi yanakusanywa kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na mapato yasiyo ya kodi yanayokusanywa na Wizara, Idara zinazojitegemea na taasisi za Serikali”, alieleza Bw. Mwandumbya.
Alisema kuwa licha ya mapato yanayokusanywa na TRA, Wizara na Idara zinazojitegemea, kiasi kinachobaki katika utekelezaji wa bajeti Serikali hukopa mikopo yenye gharama nafuu au mikopo ya kibiashara ambayo ni takribani asilimia 40 ya bajeti yote.
Alisema Serikali hufanya maamuzi ya kukopa ili kutekeleza mipango iliyojiwekea ikiwemo ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ambayo ikikamilika inafungua fursa nyingine za kiuchumi kwa Sekta binafsi kukua na hatimaye kuzalisha mapato zaidi.
Bw. Mwandumbya alibainisha kuwa inapotokea kuna eneo ambalo halijafanikiwa katika ukusanyaji wa mapato hata kama lilipangiwa kiwango kidogo cha mapato, huathiri utekelezaji wa bajeti ya Serikali.
Hivyo aliwataka wataalamu walioshiriki semina hiyo kuwa chachu kwa wengine katika maeneo yao kwa kuwajengea uwezo ili kuleta ufanisi na kuhakikisha kuwa taratibu stahiki zinazingatiwa katika ukusanyaji na usimamizi wa mapato ya Serikali.
Kwa upande wake mshiriki wa semina hiyo, Bi. Rose Werema, kutoka Mahakama ya Tanzania alisema wanaishukuru Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuandaa mafunzo hayo kwa kuwa yatawasaidia kuweka mikakati ambayo itawezesha kufikia malengo ya ukusanyaji wa mapato kulingana na vyanzo vilivyoainishwa.
“Tumeweza kupitishwa katika malengo ambayo Serikali imeweka kwa ajili ya kuweza kuendesha huduma zake mbalimbali na katika hayo tuna sehemu ya kuweza kuchangia ili kufanikisha lengo la Serikali”, alisema Bi. Werema
Wizara ya Fedha na Mipango imeandaa semina hiyo ikiwa ni moja ya jukumu lake katika kusimamia mapato ya kodi na yasiyo ya kodi na pia kutoa fursa ya wadau kubadilishana mawazo na uzoefu katika ukusanyaji wa mapato hususani yasiyo ya kodi.