Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wadau wa Madini Tumieni Teknolojia ya Kisasa - Majaliwa
Oct 26, 2023
Wadau wa Madini Tumieni Teknolojia ya Kisasa - Majaliwa
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofunga Mkutano wa Kimataifa wa Madini na Uwekezaji Tanzania (TMIF) wa 2023 kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam, Oktoba 26, 2023.
Na Ofisi ya Waziri Mkuu

Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa ametoa wito kwa wadau wa madini kujielelekeza katika kutumia teknolojia za kisasa katika uchimbaji madini ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazotokana na uchimbaji usio endelevu.

 

Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Oktoba 26, 2023) katika Hafla ya Kufunga Mkutano wa Kimataifa wa Madini na Uwekezaji Tanzania (TMIF) wa mwaka 2023. Waziri Mkuu amefunga mkutano huo kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi.

 

Mheshimiwa Majaliwa amewataka wadau hao waweke mikakati ya kuimarisha kaguzi katika masuala ya afya, usalama na utunzaji wa mazingira dhidi ya uharibifu unaoweza kuepukika katika shughuli za utafiti, uchimbaji na uchenjuaji wa madini.

 

Pia, Waziri Mkuu amesisitiza wadau mbalimbali waunganishwe na kuweka mikakati ya kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya madini kwa kufanya tafiti za madini mkakati, madini ya viwanda na madini ya metali.

 

Mheshimiwa Majaliwa amesema kutokana na uwekezaji katika Sekta ya Madini kuhitaji mitaji mikubwa, hivyo ametoa rai kwa taasisi za kifedha kuweka mazingira nafuu ya taarifa za kutoa mitaji ya kuendeleza miradi ya madini.

 

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amewataka wadau wa madini waendelee kuunga mkono juhudi za dhati za Serikali ili kuiwezesha Sekta ya Madini kukua na kutoa mchango mkubwa kwenye Pato la Taifa.

 

Pia, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wadau hao wa sekta hiyo kuwa, Serikali itazingatia ushauri na mapendekezo yaliyotolewa ili kuendelea kuboresha zaidi mazingira ya uwekezaji katika sekta ya madini nchini.

 

Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema kupitia mkutano huo wamepata nafasi ya kujifunza na kuelewa fursa nyingi za uwekezaji na namna bora ya kuendeleza sekta hiyo ya madini ikiwemo utafutaji, uchimbaji, uchenjuaji na kuongeza thamani ya madini kwa kuzingatia uhifadhi na utunzaji wa mazingira.

 

Mkutano huo wa siku mbili ulioanza Oktoba 25 hadi 26, 2023 umehudhuriwa na wadau zaidi ya 1,500 wanaowakilisha makampuni makubwa ya madini kutoka katika mataifa 75 uliambatana na maonesho ya shughuli mbalimbali za sekta ya madini yakijumuisha mabanda zaidi 60.        

 
 

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi