Waziri wa Nishati, Mhe.January Makamba ameahidi kupeleka umeme kwenye migodi ya wachimbaji wadogo katika Kijiji cha Wisolele ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu ikiwa ni utekelezaji wa moja ya vipaumbele vya Wizara ya Nishati katika kupeleka umeme kwenye maeneo ya uzalishaji ikiwemo migodi.
Waziri wa Nishati aliitoa ahadi hiyo Julai 18, 2022 wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga baada ya kufika katika eneo hilo na kujionea shughuli za uchimbaji na uchenjuaji madini zinazofanyika kwa kutumia mafuta ambapo wachimbaji hao walilalamika kuwa ni kubwa.
“Serikali baada ya kujua mahitaji ya umeme katika maeneo kama haya tukaweka mpango wa kuleta umeme kwenye maeneo ya uzalishaji ikiwemo migodi na Wisolele ni mojawapo, mpango wa manunuzi upo hatua ya mwisho na tunatarajia mwisho wa mwezi huu tutamtangaza Mkandarasi atakayeleta umeme hapa,” alisema Makamba
Alisema kuwa, ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu kazi ya uwekaji miundombinu ya umeme itakuwa imeshaanza na Serikali imetenga Shilingi milioni 336 kupeleka umeme kwenye eneo hilo.
Ili kuwasogezea huduma wachimbaji hao, alisema kuwa, TANESCO imeanzisha mfumo wa viunga vya huduma ambapo maeneo yenye watu wengi wanaweka gari na watumishi kwa masaa 24 ili zinapotokea changamoto iwe rahisi kuwahudumia wananchi ndani ya muda mfupi na Wisolele ni moja ya viunga hivyo.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Nishati alitoa agizo kwa TANESCO kuhakikisha kuwa ndani ya siku 14 wanawaunganishia umeme wateja wote walioomba kuunganishiwa huduma hiyo katika Kata ya Kagongwa wilayani Kahama, baada ya wananchi wa eneo hilo kulalamika kuwa wanachelewa kuunganishiwa umeme licha ya hatua za maombi kukamilika.
Aidha, Waziri wa Nishati pia alitembelea Shule ya Sekondari Queens of Family kwa lengo la kukagua mtambo wa bayogesi unaotumika kupikia shuleni hapo.
Akiwa shuleni hapo, alielezwa changamoto za uendeshaji wa mtambo huo ikiwemo ukosefu wa mitungi maalum ya kuhifadhi gesi pindi inapozalishwa kwa wingi, ukosefu wa vifaa vya kufanyia marekebisho na kukosa uwezo wa kuboresha na kupanua mradi huo ili kuweza kukidhi mahitaji hivyo Shule hiyo inalazimika pia kutumia kuni na mkaa badala ya bayogesi pekee.
Waziri wa Nishati aliahidi kuzitatatua changamoto zilizotajwa kupitia kwa Wakala wa Nishati Vijijini ili shule hiyo iendelee kutumia nishati ya bayogesi pekee ikiwa ni moja ya vipaumbele vya Wizara ya Nishati katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia.
Waziri wa Nishati anaendelea na ziara ya siku 21 ambayo imelenga kusikiliza maoni na kero za wananchi na kuzitatua, kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia pamoja na kukagua miradi mbalimbali ya nishati.