Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waagizwa Kujenga Mizani Barabara ya Dodoma-Babati
Aug 07, 2017
Na Msemaji Mkuu

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi. Joseph Nyamhanga, akikagua sehemu ya barabara ya Mela – Bonga (km 88.8), inayojengwa kwa kiwango cha lami mkoani Manyara.

Na. Mwandushi Wetu

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Joseph Nyamhanga, amewaagiza Mameneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Dodoma na Manyara kuhakikisha wanatafuta eneo la kujenga kituo cha mizani ili kudhibiti madereva wanaozidisha uzito katika barabara ya Dodoma- Babati yenye urefu wa kilometa 263 inayojengwa kwa kiwango cha lami.

Akizungumza katika eneo la Bonga, mkoani Manyara Mhandisi Nyamhanga, amesema kuwa barabara hiyo ambayo inatarajiwa kukamilika baadae mwezi huu inahitaji uwepo wa mizani kwa haraka ili kudhibiti magari yanayozidisha uzito na kuharibu barabara.

"Hakikisheni mnatafuta eneo la kujenga mizani ndani ya miezi miwilli ambapo wakandarasi bado wapo hapa ili iwe rahisi kwenu kumtumia mmoja wa wakandarasi hawa kuweza kujenga kituo hiki haraka, uwepo wa mizani hii utasaidia kudhibiti magari makubwa yanayozidisha uzito", amesema Katibu Mkuu Nyamhanga.

Aidha, Nyamhanga amewaagiza mameneja wote nchini kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya watu wote wanaopitisha mifugo katika barabara ili kudhibiti uharibifu wa barabara.

[caption id="attachment_8635" align="aligncenter" width="692"] Ujenzi wa barabara ya Dodoma – Babati kwa kiwango cha lami sehemu ya Mela – Bonga (km 88.8), ukiendelea.[/caption]

Amewataka madereva wote nchini kuendesha magari yao kwa tahadhari na kuzingatia alama za barabarani ili kudhibiti ajali zinazoepukika.

Katibu Mkuu Nyamhanga ametoa wito kwa wananchi wanaoishi kando ya barabara hiyo kuhakikisha wanatumia fursa ya kukamilika kwa barabara hiyo kwa ajili ya kuleta maendeleo katika maeneo yao ili kukuza uchumi kwa familia zao na Taifa kwa ujumla.

Amemataka mkandarasi wa sehemu ya barabara ya Mela - Bonga (km88.8) kuhakikisha anakamilisha kazi zilizobaki kwa wakati na kwa viwango vilivyo kwenye mkataba

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mahandisi. Joseph Nyamhanga, akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Manyara, Mhandisi. Bashiri Rwesingisa (kulia), na mkandarasi wa Kampuni ya China Railway Seventh Group Co. Ltd anayejenga sehemu ya Mela – Bonga (km 88.8), mkoani Dodoma.

Katika hatua nyingine, Nyamhanga ametembelea na kukagua barabara ya Mayamaya- Mela (km 99.35) kwa kiwango cha lami na daraja la Kelema lenye urefu wa mita 205 na kuridhishwa na ujenzi wake na kumtaka mkandarasi wa mradi huo kukabidhi mradi huo ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu.

Kwa upande wake, Mhandisi Mshauri wa barabara ya Mayamaya- Mela (km 99.35), Leornado Licari,  amemhakikishia Katibu Mkuu huyo kumaliza mradi huo kwa wakati kwani kazi  zilizobaki kwa sasa ni ndogo kama kumaliza tabaka la mwisho la lami na uwekaji wa alama za barabarani.

Barabara ya Dodoma- Babati (km 263) ni sehemu ya barabara kuu ya kaskazini (Great North road), inayoanzia Capetown nchini Afrika Kusini hadi Cairo nchini Misri ambapo hapa nchini barabara hiyo inayopitia Tunduma mkoani Mbeya, hadi Namanga mkoani Arusha ina urefu wa kilomita 1500, hivyo kukamilika kwa sehemu ya barabara ya Dodoma – Babati (km 263), kunaiunganisha barabara yote kutoka Capetown hadi Cairo yenye urefu wa kilomita 100,000 kwa kiwango cha lami.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi